Na ANNA RUHASHA
WANAWAKE wa Kata ya Nyamapande wilayani Sengerema wamelalamikia tatizo la uhaba wa maji kwa kulazimika kuyafuata mbali jambo ambalo limekuwa likihatarisha ndoa zao.
Akizungumza kwa niaba ya wanawake wenzake, Leticia Francis alisema wamekuwa wakilazimika kuamka saa 6.00 usiku na kuvizia maji visimani hivyo kuwaacha waume zao wamelala na kukaa huko saa nane wakisubiri kuchota maji.
Kwa mujibu wa wananchi hao, jambo hilo limeanza kuzua migogoro katika ndoa zao.
“Hili limeleta taabu sana baadhi yetu wamekuwa wakipigwa na waume wao wakituhumiwa kujihusisha na vitendo vya mapenzi kwa kisingizio cha kufuata maji.
“Ni tatizo kubwa kwa wanawake tunawaacha watoto na waume zetu na siku nyingine unakwenda nakukosa maji pia kwa kuwa wahitaji ni wengi hivyo kisima kinazidiwa uwezo,” alisema.
Diwani wa Kata ya Nyampande, Kaswahili Goerge (CCM) alikiri kuwapo changamoto ya upatikanaji wa maji katika kata hiyo.
Alisema wamekuwa wakitegemea visima viwili virefu vya maji ambavyo ni mali ya watu binafsi.
Alisema walikwisha kuwasilisha jambo hilo kwa mkugugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema na imani yake ni kuwa hatua zimeanza kuchukuliwa kukabiliana na changamoto ya uhaba wa maji.
“Tatizo la maji hapa nikubwa kuliko yote, kuna visima viwili tu vinavyohudumia pia halmashauri imeanza kutuletea maji kwa kutumia boza na matanki yapo wananchi waweze kununua kwa ndoo sh 50 ili kupunguza changamoto za kuvunjika kwa ndoa,” alisema Kaswahili.
Alisema serikali katika bajeti ya mwaka 2017/2018 imepanga kuanza kusambaza mabomba ya maji kutoka kwenye mradi mkubwa wa maji ambao ulizinduliwa na Rais John Magufuli hivyo kuwataka wananchi kuwa na subira.