22.1 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

WANAWAKE WAJIFUNGULIA PORINI

Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi.

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA 

WAKAZI wa Kijiji cha Zepisa, Kata ya Hombolo Bwawani Manispaa ya Dodoma, wamemwomba Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi, awasaidie ili waweze kupata huduma za afya kutokana na kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo hivyo wakati mwingine kujifungulia porini.

Wakizungumza na MTANZANIA juzi kijijini hapo, walisema kijiji hicho kipo umbali wa kilomita zaidi ya 50 kutoka Dodoma Mjini na wamekuwa wakitembea zaidi ya kilomita 10 kufuata huduma za afya katika Zahanati ya Nunge iliyopo Hombolo.

Leah Musa alisema ameshajifungulia mara mbili porini sababu zikiwa ni kurushwarushwa na pikipiki wakati akipelekwa katika kituo cha afya ili kujifungua.

“Nikiwaangalia watoto wangu huwa naona huku nipo porini kabisa japo wanasema tupo Manispaa tusaidiwe tuweze kupata zahanati hapa tunapata shida sana wakati wa kujifungua wengi tunajifungulia maporini.”

Naye Mwajuma Issa (80), alisema amewasaidia kujifungua zaidi ya kina mama 200 katika kijiji hicho kutokana na kukosekana kwa kituo cha afya.

“Nimechoka kuzalisha watu kienyeji, sasa umefika wakati wa kupatiwa na sisi zahanati ili tujifungue vizuri, kiufupi sisi tumesahaulika katika kila kitu,” alisema.

Kwa upande wake Zuhura Manyasi, alisema mimba yake ilipofika miezi 8 ilibidi ahamie kwa ndugu zake Dodoma Mjini kutokana na kuogopa kumpoteza mwanawe au yeye mwenyewe.

MTANZANIA lilimtafuta Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Kunambi ambaye alikiri kijiji hicho kutokuwa na zahanati na kuahidi suala hilo kulighulikia ili waweze kupata huduma za afya.

“Pale ujenzi ulishaanza wa zahanati na ulifikia katika hatua ya jamvi, sasa ngoja tujue tunafanyaje, maana na mimi ni mgeni lakini wale wana shida na kule ni mpakani mwa Manispaa na Wilaya ya Bahi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles