25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wanawake Mtwara wampelekea kilio cha Kiingereza Prof. Mwandosya

SARAH MOSSI NA FLORENCE SANAWA, MTWARA

WANACCM na baadhi ya wanawake wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wamedai licha ya kuwapo viwanda vingi vinavyoendelea kuzinduliwa katika manispaa yao, lakini hawapewi ajira kwa madai hawajui lugha ya Kiingereza.

Wakazi hao walitoa kilio chao jana katika Ofisi ya CCM Mtwara Mjini, mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, mara baada ya kumaliza kazi ya kutafuta wadhamini wa chama chake, ikiwa ni sehemu ya kutimiza masharti ya kuwania urais ndani ya chama hicho.

Wananchi hao wa Mtwara walitoa kilio hicho baada ya Profesa Mwandosya kuwapa nafasi kueleza yanayowasibu moyoni ili atakapopata nafasi ya kuingia Ikulu aweze kuyatatua kwa haraka matatizo yao.

“Sisi viongozi tunafikiri tuna hekima na busara na kila tunachosema tunafikiri tunawawakilisha, hivyo si hekima, busara mnayo ninyi wananchi na sasa ningependa kusikia kutoka kwenu nini niwafanyie nikifika Ikulu?” alisema Profesa Mwandosya, ambaye ameendelea kuchanja mbuga katika mikoa ya Mtwara na Lindi akitafuta wadhamini.

Mara baada ya kupewa nafasi hiyo, alisimama mmoja wa wanachama wa CCM, Mwamvua Nalinga, aliyesema anawawakilisha wanawake wenzake, akilalamika wananchi wengi kukosa ajira viwandani kwa madai hawajui Kiingereza, licha ya kuwa na ujuzi.

“Tunaomba, hapa kuna kampuni kibao, lakini ukienda kuomba kazi unafanyiwa interview (usaili), kwa Kiingereza na sisi hatujui.

“Mfano mimi ni fundi makenika, nina ujuzi na uwezo wa kazi, lakini sipati kazi sijui lugha, lakini yule anayeajiriwa ambaye anajua Kiingereza hana ujuzi wala uwezo wa kazi,” alisema Mwamvua.

Mwananchi mwingine alikuwa ni kijana Alli Matunda, ambaye alimtaka Profesa Mwandosya atakapoingia Ikulu kuweka mwongozo ili kuwafanya wafungwa wanaoingia na kutoka gerezani kuyapenda maisha yao na si yale ya gerezani.

Ferdinand Mahendeka, alisema licha ya kuwapo kwa Hospitali ya Rufaa mkoani Mtwara, lakini bado haiwasaidii wananchi, kwani hakuna dawa, vifaa pamoja na matibabu kuwa duni.

“Zahanati ya Likombe imepewa hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya, lakini haina wodi, madaktari, vifaa tiba na hakuna dawa, tunaomba ukipata nafasi kwenda Ikulu tuboreshee hilo,” alisisitiza.

Naye Hassan Daima alimwambia Profesa Mwandosya kuwa ahadi ni deni, kwani wananchi wa Mtwara wameahidiwa sana, lakini hakuna kinachofanyika na kumtaka kutimiza ahadi alizowaahidi pindi akiwa Rais.

“Ahadi ni deni, Mtwara tuliahidiwa mambo mengi, lakini hakuna, ahadi zako naomba uzitimize ili na sisi tujisikie vizuri,” alisisitiza.

Akijibu hoja hizo, Profesa Mwandosya alisema amerekodi vilio vyote vya wakazi wa Mtwara na kusisitiza amezingatia na atavifanyia kazi.

Awali akizungumza na wanaCCM waliofika kumdhamini, Profesa Mwandosya alisema ana uhakika Oktoba mwaka huu mambo yatakuwwa mazuri kwake.

Aliwashukuru wana CCM wote waliojitokeza kumdhamini, licha ya idadi ya waliojitokeza kuongezeka ikilinganishwa na idadi iliyowekwa na chama.

“Mmenidhamini pengine wengine ni mara yenu ya pili na wengine hamjapata kuniona, mmeniona na kunisikia kwenye magazeti, nitawalipa imani kama mlivyoniamini.

Profesa Mwandosya aliwasili mkoani hapa jana asubuhi saa 05:11 na kupokelewa na Katibu wa Vijana wa CCM, Joyce Mwenda pamoja na wanachama wa CCM waliobeba vipeperushi vilivyosomeka “Profesa Mwandosya, Tanzania Mzalendo Kwanza, Uzalendo wako ndiyo silaha inayokupeleka Ikulu, Mtwara tunakuamini, tunakuhitaji”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles