31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

January afunika Ruvuma

Na Dennis Luambano, Ruvuma

NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, anayeomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuteuliwa kugombea urais, jana alipata idadi kubwa ya wadhamini wanaofikia 3,550 mkoani Ruvuma.

January, ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, alipata idadi ya wadhamini hao ambao ni wanachama wenzake wa CCM siku moja tu baada ya kupata idadi ya wadhamini zaidi ya 700 katika mikoa ya Iringa na Njombe.

Akizungumza katika ofisi za CCM Mkoa wa Ruvuma baada ya kuwasili saa 11:28 asubuhi, huku msafara wake ukiongozwa na pikipiki zaidi 100 na basi lake lililopambwa kwa picha zake, January alisema amefarijika na maelfu ya wanachama wenzake waliokwenda kumdhamini.

“Kwa kweli nimefarijika sana na umati mkubwa uliokuja kunidhamini na kuja kunisikiliza. Leo (jana) hii kwangu ni siku ya historia,” alisema January.

Kutokana na idadi ya watu kuwa kubwa na kusababisha ukumbi wa CCM kufurika, ilimlazimu January aombwe na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, kwenda kuzungumza nje ya ofisi hizo.

“Idadi ya watu ni wengi, leo (jana) umepata wadhamini 3,550 na wengine walitaka kuendelea kukudhamini, lakini ukizungumza tunaomba utoke nje ya ukumbi ili kila mwana CCM aliyekuja hapa aweze kukusikiliza,” alisema Oddo.

Baada ya kutoka nje ya ukumbi huo na kuanza kuhutubia maelfu ya wanachama wa CCM, January aliendelea kuwaomba wana CCM wenzake waliotia nia ya kuteuliwa kugombea urais kuacha siasa za kuchafuana na badala yake waonyeshe ukomavu wa kisiasa.

“Tangu nilipotangaza nia na kuanza kuomba wadhamini mikoani sijamtukana wala kumkebehi mtu kwa sababu nikifanya hivyo nitakuwa nawapotezea muda nyie mliokuja kunisikiliza, kisha mkiondoka hapa mtanidharau mimi.

“Tunahitaji kufanya siasa za staha na kistaarabu kwa sababu akipatikana mgombea mmoja kutoka CCM sisi ndiyo tutakaopanda majukwaani kumnadi, kwa hiyo tukianza kupakana matope kipindi hiki tutashindwa kula matapishi yetu wenyewe wakati wa kampeni.

“Kumbukeni kutuangalia sisi tuliotia nia sasa hivi kwa namna tunavyozungumza sasa hivi au namna tunavyoomba wadhamini mikoani, iwe kwa kuchafua wengine au kwa kutoa rushwa, ndivyo tutakavyoongoza nchi,” alisema January.

Alisema kama CCM ikimteua kuwa mgombea kisha akashinda nafasi ya urais ataongoza nchi kwa weledi mkubwa utakaomfanya kila Mtanzania ajisikie fahari.

“Mimi nimekulia ndani ya CCM, nina maarifa, uwezo na nikiteuliwa nitahakikisha tunashinda uchaguzi kwa urahisi na nitaongoza nchi kwa weledi, sitayumba na matatizo ya wananchi nayajua na majawabu mapya ya kuyatatua nayajua, kwa kuwa nchi inahitaji kuongozwa kisasa.

“Rais Jakaya Kikwete aliachiwa madaraka ya urais na vizazi vya juu yake, kwa hiyo na yeye lazima aachie madaraka kwa vizazi vya chini yake kwa mtindo wa kupokezana vijiti, kwa hiyo wa chini yake si mwingine bali ni mimi,” alisema January.

Kuhusu matatizo ya Ruvuma, alisema kama akiteuliwa na CCM kugombea urais kisha akashinda urais atayashughulikia, mathalani ndani ya miaka mitano atahakikisha mkoa huo unaunganishwa katika Gridi ya Taifa na kuondokana na matatizo ya mgawo wa umeme.

“Nimekuja Ruvuma kwa kutumia basi ili nijifunze zaidi matatizo ya hapa, pia najua Ruvuma kuna mgawo mkubwa wa umeme kutokana na kutounganishwa katika Gridi ya Taifa, nitahakikisha mnaunganishwa ili muondokane na kero hiyo.

“Pia nitahakikisha hospitali ya mkoa inapanuliwa ili iweze kuhudumia wagonjwa wengi zaidi na nitahakikisha matatizo ya wakulima yanatatuliwa, mfano mkulima wa mahindi akienda kuuza mazao yake inabidi alipwe fedha zake hapo hapo na siyo kusubiri siku nyingine,” alisema January.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles