24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wanavyuo waonywa kuhusu vidhibiti mimba

Na Yohana Paul, Mwanza

Wanafunzi wa Vyuo hususan mabinti wameshauriwa kwenda kwenye vituo vya afya na hospitali kupata ushauri wa Daktari juu ya matumizi sahihi ya vidhibiti mimba ikiwemo sindano, vidonge na  vipandikizi na kuacha kutumia kwa mazoea ili kuepuka madhara ya kiafya.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wanafunzi wa Udaktari Chuo Cha Katoliki cha Afya Bugando (TAMSA-CUHAS), James Mushi, wakati wa mahojiano maalumu na Waandishi wa Habari kuelezea mikakati ya Tamsa katika kudhitibiti mimba zisizotarajiwa vyuoni.

Mushi amesema, kabla ya kutumia uzazi wa mpango ni vyema binti akafuata ushauri wa wataalamu wa afya ili kuzingatia matumizi sahihi na kupata uelewa wa njia zote za uzazi wa mpango, faida na madhara yake, uelewa ambao utamsaidia kufanya uchaguzi sahihi wa njia ya kutumia.

“Inakuwa vibaya sana kama unaamua kutumia njia ya uzazi wa mpango kwa sababu umemuona rafiki yako ametumia, bila kujua ni kwa nini mwenzio ameamua kutumia, ni lazima kujua njia unayotumia utaitumia kwa muda gani, ukishajua hapo sasa utaamua utumie njia ipi pale unaposubiri muda wa kupata mtoto.

“Kiuhalisia wanavyuo wengi bado hawapo kwenye ndoa, iwapo wapo kwenye mahusiano wanaweza kutumia vidhibiti mimba, na tumekuwa tukihamasisha matumizi ya kondomu kama njia rahisi na sahihi kwa vijana kwa kuwa haina madhara yeyote ya kiafya na kiuhalisia wanavyuo wengi hawana mahusiano ya kudumu.

“Ingawa tunahamasisha kondomu kama kinga ya mimba na magonjwa ya zinaa, vijana wasikurupuke na wasiendeshwe na hisia za mwili, na kwa wale wanaohitaji kuzuia mimba kwa muda mrefu waende kwenye vituo vya afya kupata maelekezo ya matumizi sahihi ya njia zingine kama vidonge na sindano,” amesema Mushi.

Amesema ni vyema vijana walio kwenye mahusiano wakakaa pamoja na kupanga njia gani rahisi na sahihi kwao kutumia kujikinga na mimba ili kama watahitaji mtoto basi wapate mtoto katika mazingira yaliyopangwa, kwani kiuhalisia wanavyuo wengi hawana mahusiano ya kudumu.

Anold Lukamba mwanafunzi wa mwaka wa nne chuo cha CUHAS-Bugando alikiri njia ambayo inatumika na wanavyuo wengi ni kondomu ili kuzuia mimba na maambukizi ya zinaa ambapo alishauri kila mmoja kujaribu kufuatilia elimu ya uzazi na kutumia njia ambayo ni rahisi kwake ili kuepuka mimba zisizotarajiwa.

Glorian Gudluck binti ambaye ni Mwanafunzi wa Mwaka wa Tatu CUHAS-Bugando alisema ingawa hayupo kwenye mahusiano lakini ikifikia akapata mchumba basi ni lazima atamuona daktari ili kupewa ushauri katika kuchagua njia sahihi ya kuzuia mimba huku akiwashauri wanafunzi kutumia kondomu ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles