28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wanasayansi wanavyoamini kuhusu kupatwa kwa jua

Mtaalamu wa Elimu ya anga(Astronomia),kutoka Chuo Kikuu Huria,Dk.Nooral Jiwaj akionyesha kifaa maalum ktakachotumika kutazama kupatwa kwa jua.
Mtaalamu wa Elimu ya anga(Astronomia),kutoka Chuo Kikuu Huria,Dk.Nooral Jiwaj akionyesha kifaa maalum ktakachotumika kutazama kupatwa kwa jua.

Na HERIETH FAUSTINE, DAR ES SALAAM

TUKIO la kihistoria linatarajia kutokea Septemba mosi,  ambapo jua litapatwa na mwezi. Hii itakuwa ni mara ya pili kutokea nchini ambapo mara ya mwisho ilikuwa mwaka 1977.

Kupatwa huko kunatokea wakati mwezi unafunika jua na kufanya mwanga wake kupungua hadi kutoonekana tena na kufikia kuwa giza wakati wa mchana.

Misingi ya kupatwa kwa jua

Kupatwa kwa jua kunatokea kama Dunia, Mwezi na Jua kukaa kwenye mstari mmoja mnyoofu yaani wakati mwezi unapita kati ya Dunia na Jua. Katika hali hiyo kuna kivuli cha mwezi kwenye uso wa dunia ambacho hakifuniki dunia yote na kufanya kupatwa kwa jua kunaonekana kwa watu wengi kama kupungua kwa mwanga wa jua.

Septemba mosi Jua litapatwa na Mwezi kuanzia saa nne asubuhi hadi nane mchana, katika Wilaya ya Rujewa mkoani Mbeya. Ni tukio ambalo litavuta wanataaluma wa anga kutoka duniani kote pamoja na wanasayansi, wanafunzi na jamii ya Watanzania ili kushuhudia jua linavyobadilika na kuwa pete ya jua.

Mtaalamu wa elimu ya anga(Astronomia)kutoka kitivo cha Sayansi na Teknolojia na elimu ya mazingira katika Chuo Kikuu Huria, Dk. Nooral Jiwaji, anasema watu wanaoishi ukanda wenye upana wa kilomita 100 unaokatisha kusini mwa Tanzania kutoka nchini Congo kuelekea Katavi, Mbeya, Ruvuma hadi Masasi na kuingia Msumbuji wataona jua la duara kama pete.

“Watu wa ukanda huo wataona jua likipatwa na kuwa umbo la pete kwa asilimia 98 kwa kifaa maalumu ambacho kinachuja mwanga wa jua,” anasema Dk. Jiwaji.

Anasema tukio la kupatwa kwa jua nchini lilitokea kwa mara ya kwanza mwaka 1962 na mara ya pili mwaka 1977 na kwamba hii itakuwa ni mara ya tatu, huku ikitegemewa kutokea tena mwaka 2031.

Dk. Jiwaji anasema kuwa tukio hilo ni nadra kutokea na ni la kipekee kwa wananchi na vijana wa Kitanzania.

Anasema kwa wananchi walio katika maeneo ya Kusini mwa Tanzania, tukio la kupatwa kwa jua wataliona kwa dakika tatu likiwa utosini.

Dk. Jiwaji anasema kutokana na tukio hilo kuwa la kisayansi zaidi, itakuwa fursa kwa wanafunzi kujifunza kwa vitendo somo la Sayansi la astranomia na kuelewa namna ya Jua, Mwezi na Dunia zilivyopangika angani hadi kusababishwa kupatwa.

“Wanafunzi wataelewa zaidi Sayansi yake kwa vile wataliona kwa macho yao wenyewe namna tukio linavyotokea na wataweza kufikiria na kuliweka akilini ili waelewe zaidi michoro wanayofundishwa ubaoni,” anasema Dk. Jiwaji.

Anasema kupitia tukio hilo jamii ya Tanzania itapata hamasa ya kukubali kuwa sayansi inaweza kueleza matukio ambayo kabla ya hapo walikuwa wakiyaogopa  huku wakiyahusisha na imani za kishirikina.

Dk. Jiwaji anasema kupitia tukio hilo, Taifa linaweza kuinua uchumi endapo litatangazwa kutokana na kuwapo kwa baadhi ya watalii kupenda kuangalia matukio ya kupatwa kwa jua.

“Nchi yetu inaweza kufaidika kiuchumi kwa kupata watalii kutoka nchi za nje ambao ni mashabiki wa kuangalia kupatwa kwa jua,” anasema.

Dk. Jiwaji anazitaka shule na taasisi za elimu kujitayarisha kwa kuwa siku hiyo itakuwa ya masomo na kuwataka walimu wajitayarishe kuwaongoza wanafunzi wao katika somo la Astronomia hasa kwa upande wa Sayansi, Jiografia, Fizikia na Hisabati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles