Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Wanariadha wanawake kutoka mikoa 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar, wanatarajiwa kuchuana katika mashindano ya riadha ya tamasha la ‘Ladies First’ kuanzia Novemba 24 hadi 26, 2023, jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo ambalo muasisi wake ni mwanariadha mkongwe, Juma Ikangaa, linafanyika kwa msimu wa tano sasa, likidhaminiwa na Shirikala Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA) na kuratibiwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 22, 2023, Dar es Salaam wakati wa kutangaza mashindano hayo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa(BMT), Neema Msitha amesema mgeni rasmi siku ya ufunguzi atakuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro.
Amesema ufunguzi rasmi utafanyika Novemba 25, pia kutakuwa na wageni mbalimbali walioshirikiana nao kuandaa tamasha hilo, akiwemo balozi wa Japani na viongozi wa juu wa JICA ambao ni wadhamini wakuu wa mashindano hayo.
Katibu huyo amesema pamoja na mashindano ya riadha, watafanya mafunzo na semina za ujasiriamali na uongozi kwa wanamichezo wote watakaoshiriki tamasha hilo.
“Tunafahamu wachezaji wanacheza lakini inafika kipindi wanastaafu, tumeona tuwape elimu hii ya ujasiliamali ili kuweza kujiokoa kimaisha hata baada ya kumaliza shughuli za michezo,”amesema.
Naye Mwakilishi Mkuu wa JICA Tanzania, Ara Hitoshi, amesema mashindano ya ‘Ladies First ni muendelezo wa kutengeneza usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake kupitia michezo.
Amesema anaamini michuano hiyo itatoa fursa kwa wanawake kufikia malengo ya usawa kwenye michezo na kuonyesha kile walichofanyia mazoezi kwa muda mrefu.
“Kupitia mashindano haya, Watanzania hasa wanawake na wasichana watapata msukumo wa kimichezo na wataongeza uelewa wao kuhusu umuhimu wa usawa wa kijinsia na uwezeshaji,” amesema Hitoshi.
Kwa upande wake mwakilishi wa Shirikisho la Riadha nchini(RT), Michael Washa, ametaja michezo itakayokuwepo siku hiyo kuwa ni kurusha mkuki, kupokezana vijiti na mbio za kuanzia mita 100, 200, 400,800, 1500, 5000 na 10,000.