27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi wazuia msafara wa Lowassa

LOWASSA MUHEZA 1Na Fredy Azzah, Korogwe

MSAFARA wa mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, jana ulizuiwa na wananchi katika maeneo mbalimbali mkoani Tanga ambao sehemu nyingine walikuwa wamebeba madumu ya maji kumwonyesha jinsi wanavyotaabika na kero hiyo.

Tukio la wananchi kusimamisha msafara wake wakiwa wamebeba madumu ya maji lilijitokeza katika eneo la Mkata wilayani Handeni ambao wananchi hao walimwambia   kuwa hiyo ni ishara tosha kwamba wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji.

Lowassa anayeungwa mkono na vyama vya NCCR- Mageuzi, CUF na NLD ambavyo vimejiunga katika   Ukawa, jana hakutumia helikopta kama ilivyozoeleka.

Badala yake alitumia gari kutoka mjini Tanga kwenda Korogwe na baadaye mkoani Pwani hali iliyosababisha   wananchi kufunga barabara mara kadhaa njia nzima, wakitaka mgombea huyo azungumze nao.

Kundi la kwanza kuzuia msafara huo lilikuwa eneo la Msanga na baadaye Muheza ambako  umati mkubwa wa  watu ulikuwa umetanda barabarani.

Awali, Lowassa alihutubia wananchi katika Chuo cha Ualimu (TCC) Korogwe kabla ya msafara wake kusimamishwa maeneo ya Michungwani, Kabuku na Komkonga mkoani Tanga.

Kutokana na umati kuwa mkubwa barabara katika maeneo hayo ilifungwa hali iliyomlazimu   Lowassa awasikilize  wananchi hao  waliotumia fursa hiyo kumweleza matatizo yao.

Eneo la Kabuku wananchi walibeba maji yenye tope na kumweleza   kwamba maji hayo ndiyo wanayotumia majumbani mwao ambayo yanawasababishia ugonjwa wa homa ya matumbo

Walisema  baadhi ya ndugu na jamaa zao walikwisha kufariki  dunia kutokana na tatizo hilo, hivyo walimtaka akiingia madarakani awasaidie kupata maji safi na salama.

Katika maeneo hayo pia alitumia fursa hiyo  kuwanadi wagombea wa ubunge na udiwani wanaowakilisha Ukawa katika kata na majimbo mbalimbali.

Mahakama wa wananchi

Katika Jimbo la Korogwe Mjini ulikuwapo  mgogoro wa wabunge kutoka vyama vya CUF, NCCR Mageuzi na Chadema, jambo lililomlazimu Lowassa kutumia kile ambacho Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe huita mahakama ya wananchi, kwa kuwahoji wananchi ni mgombea yupi wanayemtaka.

Wagombea hao, Rose Lugendo (NCCR,Mageuzi), Amani Hemed Kimea (Chadema) na Masoud Mohamed (CUF) walipewa dakika tatu kueleza matatizo ya wananchi wa jimbo hilo.

Baada ya kila mmoja kujieleza, Lowassa aliwahoji wananchi hao mgombea wanayemtaka ndipo umati ukalipuka kwa shangwe wakisema wanamtaka Kimea wa Chadema.

Asisitiza uamuzi mgumu

Akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara  a kwenye Uwanja wa Chuo cha Ualimu Korogwe (TCC),   Lowassa alisema kuna mambo ambayo yakifanyiwa uamuzi yatasaidia kusukuma maendeleo ya wananchi.

Wakati mwingine kufanya uamuzi ni jambo zuri kwa vile  ni rahisi kufanya marekebisho endapo uamuzi huo utabainika baadaye kuwa na kasoro kuliko kukaa kimya huku wananchi wakiendelea kuteseka, alisema.

Alisema Serikali iliyopo madarakani imeshindwa kuchukua uamuzi wa kufufua Bandari ya Tanga ambayo ingesaidia kuifufua reli ya Tanga-Arusha   na viwanda vilivyo mkoani humo.

Lowassa alisema hatua hiyo ingesaidia kuleta maendeleo   na kuinua uchumi wa watu wa Tanga na kutoa ajira kwa vijana.

“Kila ninapokuja Tanga nasononeka kwa sababu Tanga ilikuwa tajiri sana, sote tunajua shida ya Tanga ni bandari, ukijenga bandari unafungua reli na kila kitu, bila bandari mambo hayawezekani.

“Nasononeka  kwa nini uamuzi wa kufufua  bandari ya Tanga haufanyiki, kwa nini tunaruhusu umasikini uendelee?

“Ndiyo maana tunasema tunataka mabadiliko ili kurekebisha hali hii, kufufua bandari na reli  watu wa Tanga wapate maendeleo.

“Ggonjwa wa kutofanya uamuzi ni mbaya sana, serikali nikatayoiunda itakuwa inakimbia spidi 120 kwa saa,” alisema Lowassa na kushangiliwa na umati wa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles