27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli: Nitafuata nyayo za watangulizi wangu

g1Na Bakari Kimwanga, Dodoma

 

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema ataongoza nchi kwa kufuata nyayo za watangulizi wake, ili kuleta maendeleo ya kweli.

Dk. Magufuli, alitoa kauli hiyo jana kwa nyakati tofauti, alipohutubia mikutano ya kampeni katika majimbo ya Isimani mkoani Iringa, Kibakwe na Mtera mkoani Dodoma.

Alisema kazi iliyofanywa na watangulizi wake, imekuwa nzuri na yenye mafanikio, hali ambayo imeifanya Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo la Milenia (MCC), kuipatia Sh bilioni 992.8 ili kuboresha sekta ya umeme.

Alisema licha ya kurushiwa maneno ya kejeli na matusi na wagombea wa vyama vingine, hatojibu kwa kutukana ila wakati wote atahimiza amani, umoja na mshikamano.

“Nitafanyakazi ya kuijenga Tanzania mpya yenye mabadiliko na maendeleo ya kweli, kwa kuanzia pale walipoishia watangulizi wangu.

“Pamoja na kejeli za kudai hakuna kilichofanyika, hata barabara za lami hawazioni wakati wanapita kila siku na  kusafiri… ama kweli shukrani ya punda ni mateke.

“Kama hakuna kilichofanyika, leo hii MCC wangetoa mamilioni ya fedha zote hizi kwa ajili ya nchi yetu… jamani ni Magufuli tu ndiyo anaweza kuwatumikia kwa dhati na moyo wangu wote bila kubagua kwa vyama, dini wala kabila,” alisema.

Ushauri

Alisema anajivunia mafanikio aliyonayo kutokana na wazee wastaafu ambao ndio watakuwa kimbilio lake wakati wote wa utawala wake.

Alisema  kama nchi isingekuwa na hazina ya wazee, kama marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa,Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela na Rais Jakaya Kikwete isingetulia…kwa sababu  busara na hekima zao zimesaidia kuleta utulivu.

“Natamka hapa baba yangu alishafariki dunia, lakini najivunia sana Mzee Mwinyi (Ali Hassan), Mkapa (Benjamin), Salim (Ahmed), Warioba (Joseph) na huyu mzee Malecela (John), watakuwa kimbilio langu kama nitachaguliwa kuwa rais.

“Wazee hawa wamekuwa viungo kwa umoja wa Taifa letu, nami ninasema hapa nitakuwa rais wa wanyonge na si wa matajiri,” alisema.

Alisema anajua kuwa anachukiwa na mafisadi na wako tayari kumnyima kura ila anamwomba Mungu amsaidie aweze kushinda kwa kura nyingi.

“Mimi ninashangaa  unakwenda kwenye shule, unakuta wanafunzi wamekaa chini halafu mkurugenzi yupo kwenye kiti… hata siku moja hujamsikia akiomba kibali kwa ajili ya kukata miti ya madawati, watumishi wa aina hii ndiyo nitakaoanza nao,” alisema.

 

Lusinde

 

Kw upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde alisema Taifa linahitaji kiongozi mwenye msimamo na si wa majaribio kama wagombea wa vyama vingine.

“Huu ni mwaka wa majonzi kwa Ukawa na hatuko tayari kuchagua kiongozi anayetia aibu hata katika kuomba kura,” alisema.

 

Malecela

Naye Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM (Bara), John Malecela, aliwataka wana CCM kuongeza kampeni za nyumba kwa nyumba kwa kuwatumia wajumbe wa nyumba kumi.

“Wana CCM nchi nzima sasa, tuanze kazi kama ilivyo kawaida yetu kampeni za nyumba kwa nyumba zishamiri kila kona ili kujiongozea ushindi kwa rais, wabunge na madiwani,” alisema Malecela

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles