Na Walter Mguluchuma-Katavi
WAKAZI wanaoishi katika Mkoa wa Katavi, wametakiwa kuacha tabia ya kusafiri kwa kutumia usafiri wa maroli kwani kwa sasa mkoa unayo mabasi ya kutosha yanayofanya safari zake kwenda katika mikoa mingine ya hapa nchini.
Wito huo ulitolewa juzi na Ofisa wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra ) wa Mkoa wa Katavi, Amani Mwakalebela, wakati wa uzinduzi wa safari za mabasi ya Kampuni ya Adventure Connection yatakayoanza safari zake kutoka Mjini Mpanda mkoani Katavi hadi Dar es Salaam.
Uzinduzi huo wa safari ulifanyika katika stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani iliyoko katika Mtaa wa Mji Mwema mjini hapa.
“Kutokana na kuboreshwa kwa barabara za mkoa huu, kumefanya wenye mabasi wahamasike na kuleta mabasi yao, hivyo ni vema wakazi wa mkoa sasa wakasafiri kwa mabasi badala ya kusafiri kwa maroli ambayo,’ alisema.
Mwakalebela aliwataka abiria waache tabia ya kuwashangilia madereva wanaoendesha mabasi kwa mwendo kasi, kwani kufanya hivyo wanahatarisha uhai wa maisha yao.
Awali kabla ya uzinduzi huo wa safari za mabasi, wajumbe wa kamati ya usalama barabarani walitoa elimu kwa madereva pamoja na abiria.
Mwenyekiti wa Usalama Barabarani wa Mkoa wa Katavi, Nassor Arfi, aliwasisitiza wamiliki wa mabasi kutoza nauli zile ambazo zimepangwa na Sumatra.
Aliipongeza kampuni hiyo kwa kuzindua safari zake za kutoka Mpanda kuelekea Dar es Salaam, kwani itakuwa ni mkombozi kwa wasafiri ambao walikuwa wakitumia siku mbili hadi tatu kuweza kufika Dar es Salaam, lakini sasa watakuwa wanatumia siku moja tu.
Meneja wa Kampuni ya Adventure, Nassor Ally, alisema kampuni hiyo imejipanga na itaendelea kuboresha huduma kwa ajili ya wateja wake kila wakati.
Alisema watakuwa wakifanya safari hizo mara tatu kwa wiki na basi zao zitakuwa zikipita katika mikoa ya Tabora, Singida, Dodoma, Morogoro hadi Dar es Salaam.