WANANCHI WATAKIWA KUACHA KUPANDA MALORI

0
1231

Na Walter Mguluchuma-Katavi


WAKAZI wanaoishi  katika  Mkoa wa   Katavi, wametakiwa kuacha tabia ya kusafiri kwa kutumia usafiri wa  maroli kwani kwa sasa  mkoa unayo mabasi ya kutosha  yanayofanya  safari zake  kwenda  katika  mikoa mingine ya  hapa nchini.

Wito huo ulitolewa  juzi na Ofisa wa  Mamlaka ya Usafiri wa  Nchi Kavu  na   Majini (Sumatra )  wa  Mkoa wa  Katavi, Amani Mwakalebela, wakati wa  uzinduzi wa safari za mabasi ya  Kampuni ya Adventure  Connection  yatakayoanza  safari zake kutoka  Mjini  Mpanda mkoani Katavi hadi Dar es Salaam.

Uzinduzi huo wa safari ulifanyika  katika stendi kuu ya mabasi  yaendayo  mikoani iliyoko katika  Mtaa wa  Mji  Mwema  mjini hapa.

“Kutokana  na kuboreshwa kwa barabara  za  mkoa huu, kumefanya  wenye mabasi  wahamasike  na kuleta   mabasi yao, hivyo ni vema wakazi wa  mkoa sasa wakasafiri kwa  mabasi   badala ya kusafiri kwa  maroli  ambayo,’ alisema.

Mwakalebela  aliwataka  abiria  waache tabia ya kuwashangilia  madereva  wanaoendesha  mabasi kwa mwendo  kasi, kwani kufanya  hivyo wanahatarisha  uhai wa  maisha yao.

Awali  kabla ya uzinduzi huo wa safari za  mabasi, wajumbe wa  kamati ya  usalama  barabarani  walitoa elimu kwa   madereva  pamoja  na  abiria.

Mwenyekiti wa  Usalama Barabarani wa  Mkoa  wa  Katavi, Nassor  Arfi,    aliwasisitiza  wamiliki wa  mabasi  kutoza  nauli zile  ambazo  zimepangwa  na Sumatra.

 Aliipongeza  kampuni  hiyo kwa kuzindua  safari   zake  za  kutoka  Mpanda   kuelekea  Dar es  Salaam, kwani   itakuwa ni   mkombozi  kwa  wasafiri  ambao  walikuwa wakitumia siku mbili  hadi  tatu kuweza  kufika  Dar es  Salaam, lakini sasa watakuwa wanatumia  siku  moja tu.

Meneja wa  Kampuni ya Adventure,  Nassor Ally, alisema kampuni  hiyo  imejipanga na  itaendelea kuboresha  huduma kwa  ajili ya wateja  wake  kila  wakati.

 Alisema watakuwa wakifanya  safari hizo mara tatu kwa wiki na basi  zao zitakuwa zikipita katika  mikoa ya  Tabora, Singida, Dodoma, Morogoro  hadi Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here