Na Renatha Kipaka, Bukoba.
BAADHI ya wananchi mkoani Kagera wametaka chanjo ya Covid -19 itolewe bila masharti kama nyingine ili kuwaondolea hofu.
Mmoja wa wananchi hao, Teresia Mgisha (40) ambaye ni mfanyabiashara wa ndizi na mkazi wa Kayanga amesema kuwa mama yake alipochanjwa katika awamu ya kwanza alimsimulia mashariti yaliyoko kwenye fomu ambayo yalimfanya aogope.
“Niseme tu kwa upande wa wawanake wanajua tunapo jifungua huwa watoto tunawapereka hospitalini wanapata chanjo na hatuna hofu kabisa sasa kwa hili mashariti yanatisha kabisa,”anasema Teresia.
Naye Teresifori Gaspar (50) mkazi wa Bukoba Mjini anasema shida kubwa ya zoezi la chanjo ya Corona ni kukosa elimu ya kutosha kutoka kwa wahudumu wa afya.
Amesema kuna watu wengine ili wachukue hatua ya kuamini chanjo hadi wamuone mtu alievaa vazi jeupe vinginevyo ni ngumu sana kuelewa.
“Niombe Serikali kupitia Wizara ya Afya kuwatumia wauguzi kutoa elimu kwa wananchi, itasaidia watu kuelewa,”anasema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Waganga Wakuu wa Wilaya zote mkoani Kagera Dk. Diocles Ngaiza alipozungumza katika kikao cha msingi cha Kamati ya Afya ya Mkoa Kagera kuwa Halmashauri ya Kyerwa ilipatiwa chanjo 5000 na hadi Septemba 27, wamechanjwa watu 1742 ambapo watumishi wa afya ni 217 na ambao wamechanjwa ni 129 ambapo nisawa sawa na asilimia 59.
“Jambo la Msingi ni kutoa elimu mfano katika Halmashauri yetu ya Kyerwa tumeweka makubaliano ya pamoja kuwa ifikapo 1 Oktoba watumishi wote wa Afya wawe wamechanjwa “amesema Ngaiza.