MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha nyingine ya wanafunzi 1,775 wa mwaka wa kwanza waliofanikiwa kupata mikopo.
Orodha hiyo mpya inafanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo hadi sasa kufikia 31,353.
Katika awamu ya kwanza, wanafunzi 10,196 wa mwaka wa kwanza walipangiwa mikopo, awamu ya pili 11,481 na awamu ya tatu 7,901.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, ilieleza kuwa orodha kamili ya wanafunzi hao inapatikana katika tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz) na pia imeshatumwa kwa vyuo husika ili kuwawezesha wanafunzi kufanya usajili na kuendelea na masomo.
“Tumekuwa tukifanyia kazi orodha za udahili ambazo tumekuwa tukipokea na kila tunapokamilisha, tunatoa orodha za wanafunzi waliopangiwa mikopo ambao wana sifa, leo (jana) tumetoa hao 1,775,” alisema Badru.
Taarifa hiyo alieleza kuwa kiasi cha Sh bilioni 427.54 zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi kwa mwaka 2017/18 na tayari Serikali imetoa Sh bilioni 147.06 kwa ajili ya robo ya kwanza ya mwaka huu.
“Fedha hizo, shilingi 427.54 ni kwa ajili ya wanafunzi 122,623 wa mwaka wa kwanza na wale wanaoendelea na masomo,” alisema Badru.
Dirisha la rufaa
Wakati huohuo, HESLB imetangaza kufungua dirisha la rufaa kuanzia leo hadi Novemba 19, 2017 ili kuwapa fursa waombaji wote ambao hawajaridhika na upangaji wa mikopo kuwasilisha rufaa kupitia vyuo walivyopata udahili.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa HESLB, alisema lengo la HESLB ni kuhakikisha wanatangaza orodha ya majina ya waombaji mikopo waliofanikiwa katika rufaa zao ifikapo au kabla ya tarehe 30 Novemba mwaka huu.
“Tunatoa wito kwa uongozi wa vyuo vyote kupokea maombi ya rufaa za wanafuzi na kuwasilisha kwa Bodi ya Mikopo kabla ya Novemba 22, mwaka huu ili kuiwezesha Bodi kutoa orodha ya waombaji waliofanikiwa katika rufaa zao ifikapo Novemba 30, 2017,” alisema Badru katika taarifa yake.
Wiki iliyopita kundi la wanafunzi waliokosa mikopo walifanya maandamano katika Ofisi za za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Wanafunzi hao walikusanyika katika Ofisi za HESLB zilizoko Mwenge jijini Dar es Salaam, wakishinikiza wapewe mikopo ili wafanye usajili kwa mwaka wa masomo 2017/18.
Maandamano hayo yalimuibua Spika wa Bunge, Job Ndugai aliyeitaka Serikali itoe tamko bungeni kuhusu suala la mikopo kwa wanafunzi wa elimu wa juu.
Katika tamko la Serikali lililosomwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alionya juu ya tabia ya baadhi ya vyuo kuchukua fedha za mikopo za wanafunzi kwa ajili ya malipo ya usajili.
Hata hivyo alisema Serikali inafuatilia kila hatua na hakuna mwanafunzi mwenye sifa atakayekosa mikopo hiyo.