28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

KAMPENI ZA UDIWANI: VIGOGO CHADEMA, CCM JINO KWA JINO

 

VIGOGO vya vyama vya Chadema na CCM, wameanza kupambana jino kwa jino katika maeneo mbalimbali wakiwanadi wagombea udiwani wao kwa nyakati tofauti sasa.

Kwa muda mrefu vigogo kutoka vyama hivyo hawakuonekana kwenye majukwaa ya kisiasa kwa sababu ya zuio la mikutano ya hadhara.

Katika kampeni zilizoanza juzi kwenye kata 46 ambazo zinafanya uchaguzi wa marudio baada ya kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), tayari kila mmoja ameanza kumwaga sera zake.

LOWASSA

Waziri Mkuu wa zamani,  Edward Lowassa amemuomba  Rais Dk.John Magufuli kusikiliza maoni ya watu juu ya mjadala wa Katiba Mpya.

Lowassa alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika uzinduzi wa uchaguzi mdogo wa udiwani kwa tiketi ya Chadema uliofanyika Kata ya Moita, wilayani hapa Mkoa wa Arusha.

Alisema upatikanaji wa Katiba Mpya na yenye ubora utasaidia baadhi ya nchi za Afrika Mashariki, ikiwemo Kenya ambayo hivi karibuni walikuwa na Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo.

Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema upatikanaji wa Katiba Mpya iliyo bora utasaidia nchi kwenda vizuri na kutoa mfano wa nchi jirani ya Kenya.

“Kuna mjadala unaoendelea kwamba iwepo Katiba ama isiwepo, naomba nichangie sehemu ndogo tu naomba mnisikilize.Ninamuomba Rais kwa heshima zote akubali asikilize maoni ya watu wengine kabla hajafanya uamuzi.

“Nchi itakwenda vizuri tukiwa na Katiba yenye ubora, Katiba yenye ubora ni kama ya Kenya, kama wasingekuwa na Katiba bora wangekuwa pabaya, wana Katiba bora wameweza kushitaki mahakamani na kadhalika, wana amani na utulivu kwa sababu wana chombo kizuri kinachowaongoza,” alisema Lowassa.

Aidha Lowassa alisema nchi inaongozwa na watu zaidi ya mmoja na hakuna chama kinachotawala peke yake.

“Nchi siku hizi zinaongozwa na watu zaidi ya mmoja, vyama vinakuwa vingi, vyama vinatawala hakuna chama kinachotawala peke yake duniani siku hizi, angalau kuna wanaopigapiga kelele pale jirani na wanakuwepo wanaruhusiwa, kwetu kuna shida ya kitu kinaitwa ‘coalition,’ nawataka leo Watanzania kutafakari uwezekamo wa kupata ‘coalition’ katika nchi yetu.

“Mimi 2015 kwenye uchaguzi wa Rais walinipa kura milioni sita, hizo walinipa wao ila walizonipa wananchi ni nyingi zaidi, wakampa Rais Magufuli kura milioni nane, kura milioni sita hazina maana yoyote, hawasikilizwi popote hawana faida yoyote wala hawaambiwi chochote, milioni nane anakuwa ni kila kitu.

“Kwa nchi nyingine kura milioni sita anapata nafasi ya kuchangia katika vitu vingine kama ni wabunge, kitu gani lakini inakuja katika suala la ujumla kwamba anaongoza siyo peke yake, anaongoza na wenzake. Kwa mfano Ufaransa ni nchi ya kibepari lakini inaongozwa kwa ujamaa kwa sababu ya aina ya wabunge walionao,” alisema Lowassa

Pia alitoa mfano wa nchi ya Marekani wakati wa kipindi cha urais wa Barrack Obama kuwa ilikuwa na tatizo kubwa la uchumi lakini alichukua njia za kijamaa kwa kuchukua fedha za umma na kuwekeza katika mashirika binafsi na uchumi ukakua.

“Nilitaka kusema ukiwa na ‘coalition’ ambayo vyama vya upinzani vitaungana, mkapata madaraka ya uongozi katika nchi ambayo inazingatia maoni ya watu wengi ni muhimu.

“Leo hii niseme kwa sababu katika Katiba ni vizuri ikafuatwa lakini katika ‘coalition’ liko jambo la msingi, vyama vya siasa ni vingi ukifika wakati wa uchaguzi unaviona na vinatumika vibaya.

“Kwa mfano Rais wa Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), marehemu Mabutu Seseseko alikuwa anaunda vyama vingi vya siasa anasubiri wakati wa uchaguzi anavilipa pesa vinamuunga mkono, tusikubali mambo kama haya. Nimelisema hili ili nichangie mjadala unaoendelea,” alisema Lowassa.

Akimnadi mgombe udiwani, Lobulu Lomnyaki, aliwaomba wananchi wamchague ili aweze kuungana na madiwani wenzake kuwaletea maendeleo.

 

MBOWE

Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alielezea namna aliyekuwa Katibu Mkuu chama hicho, Willibrod Slaa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba walivyousaliti Ukawa katika Uchaguzi Mkuu wa waka 2015.

Mbowe alitoa kauli hiyo mjini hapa jana, wakati akimnadi mgombea udiwani wa Chadema, Kata ya Reli, Antony Kwesi katika uwanja wa Shule ya Msingi Serengeti uliopo Manispaa ya Mikindani mkoani Mtwara.

Uchaguzi wa Kata ya Reli unarudiwa baada ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Philipo Momba kufariki dunia.

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema pamoja na kwamba Profesa Lipumba alijiweka kando katika uchaguzi huo, chama chake kilipata wabunge wengi kutoka bara kuliko kipindi chochote ambacho mchumi huyo alipata kugombea urais.

“Mwaka 2015 tuliunganisha nguvu zetu, tukasema Lipumba njoo tuunganishe Watanzania, akateleza na Slaa naye akateleza nikasema mimi nakomaa.

“Sasa wale ambao tuliwaamini kuwa tuko nao safari moja, kumbe tuna safari tofauti…ndugu zangu sikuja kumkashifu mtu, nimekuja kujenga hoja huyu Maftah Nachuma (Mbunge wa Mtwara Mjini), tukampitisha agombee na Chadema tulikuwa tuna mgombea wetu mzuri na msomi, tukamwomba akubali Maftah agombee aliumia kwa kuwa alikuwa amejiandaa.

“Sasa leo  huyu Maftah ambaye ametusaliti kwa kuwa upande wa CCM, si asimamishe tu mgombea udiwani wa CCM? Hivyo siwezi nikamsifu mtu msaliti.

“Huyu Lipumba naye anaenda kukipasua CUF leo akisaidiwa na Ofisi ya  Msajili wa Vyama vya Siasa na Spika, amesahau alisaliti akakimbilia Rwanda, wenzake tukapambana mpaka tukapata wabunge wengi zaidi.

“Lipumba sina ugomvi naye, nikisema namheshimu nitakuwa ng’ombe…msomi wa ajabu kweli, kusoma si wingi wa vyeti bali ni namna ya kutumia elimu, ” alisema Mbowe.

Alisema kazi kubwa ya CCM ni kupasua CUF na si kwamba hawakijaribu Chadema, bali kila wakijaribu wanagonga ukuta.

“Simwogopi mtu yeyote isipokuwa Mungu tu na ninausimamia ukweli. Kwa bahati mbaya walidhani Chadema ni laini lakini wakipiga huku na kule mzigo unagoma.

“Siku nikiingia kaburini ndiyo watakiua Chadema si sasa, “alisema Mbowe.

Aliwataka wananchi kuacha ushabiki bali wajadili mustakabali wa taifa.

“Tuache shamrashamra na ushabiki tujadili mustakabali wa taifa letu. Nimekuja kuwaunganisha wananchi wa Mtwara.

“Siasa ni maisha hivyo nampa ujumbe JPM atuache sisi tuzungumze pamoja na kwamba yeye anasema tupige kazi lakini anafanya siasa,” alisema Mbowe.

Akizungumzia umuhimu wa kupatikana kwa Katiba Mpya alisema uko palepale kwa sababu hata Mwalimu Nyerere (Julius) alipata kusema kuwa kwa Katiba hii mtawala akiamua kuwa dikteta anaweza kwa sababu rais amepewa madaraka makubwa.

“Kenya walilikataa jambo hili wakafanya mabadiliko ya Katiba ndiyo maana hakuna kiongozi anayepewa cheo bila kupigiwa kura hivyo Chadema ikiingia madarakani tutaondokana na hivi vyeo vya kupeana, “alisema Mbowe.

MWIGULU

Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmshauri Kuu (NEC) ya CCM, Mwigulu Nchemba, amewashangaa wanasiasa wanaodai kuna utawala wa kidiketa hapa nchini kwa kusema wameshindwa kutofautisha dhana ya udikteta na utawala wa sheria.

Mwigulu aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua kampeni za  CCM katika uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Saranga, wilayani Ubungo.

Alisema Rais Dk.Magufuli anajali zaidi utawala wa sheria ndiyo maana aliamua kuwa na mahakama ya mafisadi na siku zote amekuwa akisimamia haki kwa kuwatetea wanyonge.

“Wanaodai kuna utawala wa kidikteta wanashindwa kutofautisha kati ya udikteta na utawala wa sheria. Nchi yetu inasimama katika misingi ya utawala wa sheria. Rais wetu ni kati ya watu makini barani Afrika katika kufuata misingi ya utawala wa sheria.

“Unasema Tanzania kuna udikteta wakati  unakunywa moja moto moja baridi. Kwenye Taifa lenye udikiteta utafanya hivyo? Unasema kuna udikiteta wakati bungeni unahudhuria .Udikteta uko wapi?” alihoji Nchemba.

Alisema lazima awe mkali kwa sababu  uonevu kwa wanyonge ulizidi.

“Leo hii Rais Dk. Magufuli hata raia akimtumia ujumbe mfupi wa kueleza malalamiko yake, lazima anaufanyia kazi ili haki itendeke. Kusaidia wanyonge ndiyo udikteta?” alihoji Nchemba ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani.

Aliwataka wananchi kupuuza kauli za wanasiasa kwa sababu Serikali imekusudia kuwaletea maendeleo.

Nchemba aliwaomba wananchi wa Kata ya Saranga kumchagua mgombea wa CCM, Haroun Mdoe ili atekeleza ilani ya chama.

“Ilani inayotekelezwa  ni ya CCM, kama mtamchagua Mdoe ataweza kuwatatulieni changamoto zenu kwa sababu anawajibika katika Serikali iliyopo madarakani.

“Mkichagua upinzani hawezi kutekeleza ilani badala yake watafanya kazi ya kuharibu  shughuli za maendeleo ili katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 waje waeleze kuwa CCM haijafanya kitu,” alisema Nchemba.

Akijinadi kwa wananchi, Mdoe alisema kata hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazotokana na kutokuwepo kwa mtu wa kuziwasilisha katika Baraza la Madiwani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles