NA FRANCIS GODWIN, IRINGA
WANAFUNZI wawili wa Shule ya Southern Highlands Mafinga, Maria Wambura na Stephen Sang, wameondoka nchini kuelekea nchini Finland kuiwakiisha Tanzania katika kongamano la mazingira la wanafunzi duniani.
Akizungumza wakati akiwakabidhi Bendera ya Taifa wanafunzi hao, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mufindi, Festo Mgina, alisema heshima ambayo shule hiyo imepata ni kubwa.
“Huu ni mwaliko wa heshima kubwa kwa wilaya yetu na mkoa, lakini kwa Taifa letu kualikwa katika kongamano kubwa kama hili la kujadili masuala ya mazingira duniani, heshima hii sisi kama viongozi tunajivunia na tunapongeza shule kwa kuteuliwa kuwakilisha Taifa,” alisema.
Aliagiza wakuu wa shule za msingi wilayani Mufindi kuhakikisha wanafika Southern Highlands ili kujifunza yale ambayo wanafunzi hao watarudi nayo.
“Tunataka elimu na maagizo ambayo yatatolewa katika mkutano huo wa dunia nchini Finland, vijana hao wakirudi basi kuweza kusambaza kwa wenzao katika shule zote za Mufindi, ikiwa ni pamoja na wakuu wa shule kufika kujifunza ili kila shule kujifunza elimu hiyo kwa faida ya mazingira ya maeneo yao,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Southern Highlands Mafinga, Kitova Mungai, alisema shule hiyo ni miongoni mwa shule wanachama wa Klabu za Mazingira Duniani na kuteuliwa kwa wanafunzi hao kumetokana na ziara ya waratibu wa kongamano hilo waliofika kupima uwezo wa klabu zote nchini.
“Tunategemea kukutana na wawakilishi kutoka nchi mbalimbali duniani kama China, Japan, Brazil, Marekani, China, Uganda, Kenya na nchi nyingine, ila tuna imani kubwa ya kuwakilisha vema Tanzania kwa sababu watoto waliochaguliwa kwenda katika kongamano hilo wana uwezo mkubwa katika elimu ya mazingira,” alisema Mungai.
Alisema watoto hao na wenzao wamekuwa mbele kuhifadhi mazingira ya shule kwa kuotesha miche ya miti na kuipeleka shuleni hapo na nyumbani kwao.
Kwa upande wao, Maria na Stephen ambao ni wanafunzi wa darasa la saba, walisema kuteuliwa kwao katika kongamano hilo si nafasi ya bahati mbaya kwa sababu wana uhakika wa kuliwakilisha vizuri Taifa na kile watakachokipata watakuja kukitumia kutoa elimu kwa wanafunzi wenzao hapa nchini.