22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi waanguka ghafla, watembeza kichapo kwa walimu

watoto(Picha kutoka mtandaoni)

NA GUSTAPHU HAULE

-PWANI
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mafia, imelazimika kuifunga Shule ya Msingi Misufini iliyopo Kata ya Kilindoni kwa siku tatu, baada ya kuzuka ugonjwa wa ajabu uliosababisha wanafunzi zaidi ya 50 kuanguka darasani na kupoteza fahamu.

Wanafunzi hao wa kike walianguka huku wengine wakipata nguvu za ajabu kiasi cha kuwapiga walimu wao.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Erick Mapunda, alisema wamelazimika kufunga shule hiyo ili kutafuta suluhu ya kumaliza tatizo hilo shuleni hapo.

Akizungumza na MTANZANIA jana kwa njia ya simu, Mapunda alisema tukio hilo lilitokea Novemba 10, mwaka huu ambapo wanafunzi 30 wakiwa darasani ghafla walianza kurukwa na ufahamu na hatimaye kuwapiga walimu wao.

Mapunda alisema kesho yake kuanzia saa mbili asubuhi wanafunzi wengine zaidi ya 18 walianza kutokewa na hali hiyo, jambo ambalo lilipoteza amani katika shule hiyo na hivyo kupoteza mwelekeo wa masomo.

“Cha kushangaza tulipotaka kuwachukua wanafunzi hao ili kuwapeleka hospitali kwa ajili ya kupata tiba, wazazi wao walipinga kwa kusema ugonjwa huo ni wakisayansi na kwamba wao wenyewe wanajua tatizo hilo,” alisema.

Alisema baada ya walimu kuambulia kipigo kutoka kwa wanafunzi wao, nao walianza kuogopa na wengine kukimbia na kujificha katika maeneo yasiyojulikana kwa kuhofia uhai wao lakini wapo wazazi ambao walijitokeza na kumudu kuwashika wanafunzi.

“Baada ya kuona hali si nzuri shuleni hapo, tulilazimika kuifunga shule hiyo kwa muda wa siku tatu ili kupisha majadiliano ya wazazi na kamati ya shule,” alisema.
Alisema majadiliano hayo yanafanyika kutokana na wazazi hao kugoma kuwapeleka watoto hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu na kama hakutakuwa na mwafaka ataifunga shule hiyo hadi muhula ujao.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo aliwataka wazazi na wanafunzi wa shule hiyo kuwa na subira wakati jitihada hizo zikiendelea kufanyika, huku akiomba ushirikiano ili kunusuru hali hiyo na kuwapa watoto nafasi yao ya kusoma katika mazingira salama.
Mwisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles