NA FLORENCE SANAWA, MTWARA
MKOA wa Mtwara umekuwa ukikabiliwa na changomoto mbalimbali za miundombinu ya elimu hali iliyochangia baadhi ya wanafunzi kushindwa kuhudhuria vipindi darasani.
hivyo kupelekea uwepo wa utoro darasani.
Shule nyingi mkoani humo zina uhaba mkubwa wa miundombinu ya vyoo hali ambayo inasababisha kuwapo kwa mlipuko wa magonjwa kutokana na vyoo vingi kuelemewa na idadi ya watumiaji hali inayoongeza changamoto kwao.
Ziko shule ambazo hazina vyoo kabisa huku nyingine zikilazimika kutumia choo kimoja na shule za jirani hali ambayo imekuwa ikihatarisha afya za wanafunzi hao kutokana na uwiano usio sawa katika matumizi ya vyoo hivyo.
Mojawapo ya shule zenye changamoto hiyo ni Shule ya Msingi Maendeleo ambapo choo cha shule hiyo kimefungwa kwa takribani miaka minne sasa kutokana na kutokidhi kwa matumizi ya wanafunzi.
MWALIMU MKUU MAENDELEO
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Maendeleo, Fabiola Haule, anasema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2007 baada ya kugawanywa Shule ya Msingi Rahaleo.
“Shule ina wanafunzi 534 ambao walihamishwa kutoka Shule ya Msingi Rahaleo baada ya idadi ya wanafunzi kuonekana kuwa kubwa katika shule hiyo,” anasema Haule.
Anasema baada ya kutengwa shule hiyo iliachwa na matundu ya vyoo mabovu ambayo waliona yanahatarisha maisha ya wanafuzi wanaosoma na hivyo kulazimika kuifunga ili kuwanusuru hali ambayo imeongeza tatizo kwa wanafunzi hao.
Mwalimu huyo anasema kwa kipindi kirefu amekuwa mstari wa mbele ili kuhakikisha shule hiyo inapata choo lakini jitihada hizo zimegonga mwamba.
“Kuna watu walitumwa na manispaa kuja kupiga picha kuonyesha jinsi hali ya miundombinu ya vyoo ilivyo, walikuja zaidi ya mara nne lakini hadi sasa sijaona juhudi zozote zikifanyika kuweza kupata vyoo katika shule yetu.
“Choo hiki ni cha muda mrefu tangu Shule ya Msingi Rahaleo ilipoanzishwa miaka ya 1970, tuliona kuwa mazingira yake ni hatarishi hali ambayo ilitulazimu kutoa taarifa katika mamlaka husika ili tuweze kupata msaada wa kutengenezewa choo.
“Kumekuwa na mlipuko wa magonjwa mbalimbali hali ambayo yamesababisha watoto kuwa watoro kutokana na kuumwa, wazazi waone umuhimu wa kuboresha mazingira ya choo ili kupunguza mlipuko wa magonjwa unaotokea mara kwa mara,” anasema Haule.
MWALIMU MKUU RAHALEO
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Rahaleo, Kulwa Gambalama, anasema shule hiyo ina wanafunzi zaidi ya 700 ina uhaba mkubwa wa vyoo huku mahitaji yakiwa ni matundu 34.
“Hadi sasa tuna matundu 18 tu ambapo 10 hutumiwa na wavulana na 8 hutumiwa na wasichana,” anasema Mwalimu Gambalama.
Anasema matundu hayo 18 yamekuwa yakitumiwa na wanafunzi zaidi ya1000 hali ambayo imekuwa ikisababisha kila baada ya nusu saa choo kuchafuka.
“Shule mbili kutumia choo kimoja ni adha kubha, mimi nina upungufu wa zaidi ya matundu 16 lakini pia namsaidia mwenzangu pamoja na usafi unaofanyika bado mazingira kwa shule zote mbili hayaridhishi.
“Mwanzoni tulikuwa na matundu saba tu, mawili yalikuwa yakitumiwa na wanaume na matano yalikuwa yakitumiwa na wasichana hali ilikuwa mbaya zaidi, wadau wawekeze pia katika ujenzi wa matundu ya vyoo ili kulinda afya za watoto wanapokuwa shuleni.
“Si suala la choo tu hata miundombinu yote ni shida mnaweza kuangalia shule yetu inavyoleta taswira mbaya kwakuwa ipo katikati ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, haileti picha nzuri kukosa choo,” anasema Gambalama.
WANAFUNZI
Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Maendeleo, Thabiti Hussein, anasema kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakikosa vipindi darasani kutokana na foleni kubwa wanayopanga kwenda kujisaidia hali ambayo inawalazimu kusubiriana badala ya kuwahi vipindi darasani.
Anasema kitendo cha shule mbili kutumia choo kimoja kinasababisha usafi wa vyoo hivyo kutofanywa kwa ufasaha hali ambayo inahatarisha afya zao kwakuwa wao ndio watumiaji wa huduma hiyo.
“Vyoo si visafi nahisi ni kutokana na wingi wa wanafunzi tunaotumia lakini kwanini manispaa haiangalii hili jambo ikalirekebisha ili kuweza kutuweka salama kiafya na kutuepusha na magonjwa ya milipuko? anahoji Fadhili.
Mwanafunzi mwingine wa darasa la saba katika shule hiyo, Mashaka Fadhili, anasema katika suala la usafi wao ndio wamekuwa wakilaumiwa kutokana na shule yao kukosa vyoo.
“Tunalazimishwa kufanya usafi na walimu wa shule ya jirani ambayo ndio yenye choo. Wanapokuta choo kichafu huwa wanatutoa darasani kwa ajili kufanya usafi, hali hii inatuathiri kwa sababu wakati mwingine tunakosa vipindi na huwa tunapewa adhabu na walimu kwa kukosa vipindi darasani,” anasema Fadhili.
Naye Saida Said mwanafunzi wa Darasa la Saba katika Shule ya Msingi Maendeleo, anasema wamekuwa wakikosa baadhi ya vipindi darasani kutokana na kukaa muda mrefu kwenye foleni hali ambayo imekuwa ikiwakatisha tamaa kutokana na kutoelewa darasani hasa wanapofika mwisho mwa vipindi.
“Hali hii huwa inatutesa sana wanafunzi wa kike kiafya kwakuwa mara zote tumekuwa tukiona aibu kujisaidia vichakani hatua ambayo imekuwa ikituletea magonjwa mbalimbali ukiwemo (UTI).
”Unaweza kwenda chooni ukakuta foleni kubwa ukasubiri ukimaliza kujisaidia na kurudi darasani unakuta mwalimu uliyemuacha hayupo yupo wa somo lingine. Hata kusoma kwenyewe huelewi unakuta wengine wameshaelekezwa wewe ulikuwa kwenye foleni ya chooni, hali hii inatutesa sana.
“Au unaweza kwenda unakuta vyoo vimefungwa hali ambayo imekuwa ikichangia uharibifu wa mazingira kwakuwa wanafunzi wengine huamua kujisaidia katika maeneo yasiyofaa,” anasema Saida.
Wanafunzi hao waniomba manispaa isikie kilo chao na kuwasaidia ili waweze kupata choo hatua ambayo itapunguza pia uchafuzi wa mazingira wa ndani ya shule na nje kutokana na baadhi ya wanafunzi kujisadia katika maeneo hayo ili waweze kuwahi vipindi darasani.
NAIBU MEYA
Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Erick Mkapa ambaye ni Diwani wa Kata ya Rahaleo, anakiri kuwapo kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa anafanya juhudi za kuwashirikisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha wanatatua tatizo hilo.