23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Hofu ya ujio wa ndoa baina ya roboti, binadamu

robot

Joseph Hiza, Dar es Salaam

MMEFAHAMIANA kwa miaka mingi sasa, na kila mmoja amemjua mwenzake kwa undani zaidi.

Mnachangia nyumba moja, kila mmoja ana mahala pake pa ajira. Iwapo hilo ni sahihi mna utaratibu wa mmoja wenu kumpitia mwenzake kazini baada ya saa za kazi ili mrudi nyumbani pamoja.

Kadhalika mnavinjari bustanini pamoja, mnakula mlo pamoja bila kujali iwapo mmoja wenu ana mlo maalumu, ambao kamwe mwenzake pengine hawezi kuutia mdomoni na kwa pamoja mnalipa bili za umeme, maji na kadhalika.

Hali kadhalika mnaonekana matembezini pamoja iwe ufukweni mwa bahari au popote pale mnapopanga kwenda. Kunani hapo? Hakuna shaka hakika mko ndani ya mapenzi mazito!.

Mnaonekana kutamani mfunge ndoa, lakini kwa bahati mbaya sana, mmoja wenu anaishi katika jamii ambayo uhusiano huo unahesabika kutokuwa wa asili na ni haramu na au uchuro.

Pamoja na mpenzi wako kuwa na pumzi na hisia kama zako na anafanya kazi na ana uwezo wa kusoma, kwa kiasi kikubwa hana tofauti sana na wewe ila bado ndoa hiyo ni kinyume na sheria.

Laiti mpenzi wako huyo angekuwa mwanadamu hata kama wa jinsia ile kama yako badala ya uroboti alio nao baadhi ya jamii zilizokuzunguka zingeivumilia au kuikubali na hata kuitetea kwa nguvu ndoa hiyo isiyokubalika mbele ya Muumba wala tamaduni nyingi zikiwamo za Kiafrika.

Wakati baadhi ya nchi au majimbo ya Marekani yamepitisha ndoa za mashoga au kuwa katika mijadala mikali kuhusu ndoa hizo, kuna hofu ya ujio wa ndoa baina ya roboti na binadamu katika siku za usoni.

Mmoja wa wanaharakati wapingao uhusiano wa kimapenzi usio wa asili nchini Marekani, Robert Broadus amesema kupitishwa kwa miswada inayohalalisha ndoa za jinsia moja, kutasababisha kuhalalishwa zile baina ya roboti na mwanadamu katika siku za usoni.

“Iwapo wanasiasa hawa wanapitisha miswada hii, kutajengwa msingi ambao hautashangaza tukishuhudia wakiruhusu au kushinikiza ndoa za wanadamu na roboti.”

Iwapo mnaona watu wawili wamependana bila kujali jinsia zao mkawaruhusu waishi pamoja nini kitashindikana kupitisha uchuro mwingine baina ya wanadamu na vitu vya kutengeneza,” Broadus, ambaye anaongoza taasisi inayopigania kulinda misingi ya ndoa za asili alisema.

Akisisitiza kile asemacho, Broadus alirejea uwezo wa baadhi ya roboti zilizoonyesha uwezo mkubwa kama wa binadamu ikiwamo kuonyesha hisia hadi kumwaga machozi.

“Kwa bahati mbaya au nzuri, tayari baadhi ya watu wanafanya ngono na roboti, alisema akirejea kile kinachoonekana midoli au wanasesere wanaotumika katika tendo hilo kwa miongo kadhaa sasa.

Anachosema mwanaharakati huyo hakina tofauti na kile ambacho watafiti wengi wa masuala ya roboti na saikolojia wanatabiri.

Miongoni mwa mifano aliyorejea Broadus kuhusu uwezo wa roboti ni Hertz.

Akiwa na macho bluu, nyusi na tabasamu la aibu, Hertz amekuwa kivutio kikubwa popote pale aendako.

Iwapo utakuwa na bahati ya kuonana naye, jaribu kupuuza mwonekano wa nyaya nyuma ya uso wake.

Iwapo utazungumza naye, zungumza taratibu na kwa sauti kubwa. Na bila kujali nini usemacho, usikasirike wakati atakapokutupia macho ya kupepesa na kukuuliza kwa kurudiarudia, “Unasema nini?”

Hertz si mwanadamu kama utakavyodhani, bali aliyeingizwa chembe ya uanadamu, akiwa ametengenezwa kwa karibu miezi minane na mtaalamu wa roboti, David Hanson.

Hanson na watengenezaji wengine wanaamini roboti ambazo tayari zinafanya shughuli nyingi zinazoweza kufanywa na binadamu siku moja zitajishughulisha na shughuli za kijamii kama vile ualimu, ndoa hadi ulinzi.

Wakati ndoa za binadamu na roboti zikionekana kama kitu kisichowezekana kwa sasa, huenda zikawa jambo la kawaida siku moja iwapo nadharia za mtafiti David Levy itadhihirisha usahihi wake.

Levy, mtafiti wa Uingereza ambaye miaka michache iliyopita alijipatia Shahada yake ya Udaktari wa Falsafa (PHd) kutoka Chuo Kikuu cha Maastricht nchini Uholanzi anaamini ifikapo mwaka 2050, roboti na wanadamu wataoana kihalali nchini Marekani.

Alitabiri Jimbo la Massachusetts litakuwa la kwanza kusafisha njia kama lilivyofanya mwaka 2004, wakati lilipokuwa kwanza kuruhusu ndoa za jinsia moja baina ya wanadamu.

Ndoa za jinsi moja huko nyuma zilionekana kuwa kitu kisichowezekana lakini kwa kadiri ya miaka ilivyosonga mbele zimekuwa jambo la kawaida katika nchi zilizoendelea na Afrika Kusini ilikuwa nchi ya kwanza Afrika kuruhusu uhusiano huo ambao ni mwiko katika jamii nyingi barani humo pamoja na kuharamishwa kwenye vitabu vya dini.

Mbali ya hayo mataifa makubwa yakiongozwa na Marekani na Uingereza yameweka suala la ndoa za mashoga kuwa kigezo cha kutoa misaada kwa mataifa masikini.

Tumeshuhudia Uganda ikinyimwa misaada baada ya kupitisha sheria inayopinga vitendo vya ushoga, ambavyo kwa mujibu wa utamaduni wa Kiafrika na vitabu vya dini zote takatifu ni haramu na dhambi.

Kadiri roboti wanavyozidi kuwa na umbo la binadamu, Levy na wataalamu wengine wa roboti ndivyo wanavyoamini watu wataanza kujenga uhusiano nao wa kimapenzi.

Wanasema haishangazi kwa sasa kuwapo watu wanaotumia midoli, hivyo kwa roboti zenye uwezo mkubwa kuliko wanasesere wasiyohuishwa chochote kuwa na hisia za binadamu ni jambo lingine.

Umbo na mwili mzuri wa kuvutia, kuwa na hisia kama za binadamu na mengine miongoni mwa roboti zitaweza ‘kuzalisha’ wenzi ambao baadhi ya wanadamu watapenda kuwaoa.

Wataalamu wanasema visababishi vyote muhimu vinavyofanya wanadamu kuangukia katika uhusiano wa kimapenzi vitapandikizwa ndani ya roboti.

Hata hivyo, Levy hatabiri kupungua kwa ndoa baina ya wanadamu wenyewe na kuzaana wala hafikirii kuwa watu wengi watachagua wapenzi wa kiroboti kuliko wanadamu wenzao.

Bali watu wenye kuendekeza mambo hayo watakuwa wale ambao huona fadhaa au haya kuhusiana na wenzao na kadhalika watu wenye matatizo ya akili.

Kwa sasa roboti wanafanya mambo mengi sawa na wanadamu kama vile shughuli za hospitali, kutunza watoto au wazee, shughuli za uchimbaji migodi, vitani na na kadhalika na miaka ya karibuni roboti aliushangaza ulimwengu wakati alipofungisha ndoa nchini Japan.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles