31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Utamaduni wa kunengua uchi mazishini washamiri Asia

Jeneza

* Wasichana huchojoa nguo na kunengua watupu

Na JOSEPH HIZA,

KUINGIA kwa utandawazi duniani kumeleta mabadiliko mengi chanya na hasi pia, ikiwa ni pamoja na kuathiri mila na desturi zilizokuwapo ikiwamo suala zima la uendeshaji mazishi katika jamii.

Mabadiliko yanayoonekana katika zama hizi mazishini kwa asilimia kubwa yana mwelekeo wa kujali zaidi mahitaji ya kimwili ya watu wanaofika msibani kuliko mahitaji ya marehemu.

Kwa kawaida katika maisha ya binadamu ana sherehe kuu tatu za msingi; ya kwanza ikiwa ni ya kuzaliwa, ya pili ndoa na ya tatu ikiwa kifo.

Hata hivyo namna ya kuzisherehekea hutofautiana kwa kutegemea mazingira yaliyozingira tukio hilo yakitegemea kama ni la furaha au huzuni.

Kwa msingi huo, sherehe za kuzaliwa na ile ya ndoa kwa kawaida hutawaliwa na furaha kwa wahusika, familia, ndugu, jamaa na marafiki zao.

Lakini kinyume na sherehe hizo kwa asilimia kubwa ile ya kifo wafiwa hawatakubali hali waliyonayo iwe ‘sherehe ya kifo’ kwa sababu moja kifo hutawaliwa na hisia za majonzi na huzuni. Huu ni ndio ukweli.

Lakini pamoja na ukweli huo, nyakati hizi za sayansi na teknolojia, ni kawaida kushuhudia mazishi yakitawaliwa na shangwe, muziki, ulevi kwa kumwaga na hivyo neema za kimwili na wafanyabiashara wa pombe.

Hufanya tukio zima liondoe dhana ile tuliyoizoea ya uwapo wa msiba mahali hapo.

Mabadiliko haya hayazikumbi tu jamii zetu za Kiafrika, bali pia katika mataifa ya Magharibi na Asia ambako bila shaka ndiko tulikoyaiga kwa gharama ya utandawazi.

Katika mataifa hayo yalianza zamani sana kwenda tofauti na maana ile ya msiba, wakienda mbali zaidi kukodi waombolezaji ili kuujaza msiba.

Hayo ni tisa, kumi katika mataifa hayo hasa Asia kuna mila ya ukodishaji vikundi vya starehe hasa vyenye wanenguaji wa nusu uchi, ambavyo havina tofauti kabisa na vile vya vilabu vya usiku vilivyoshamiri katika mataifa ya magharibi.

Wanenguaji hao wanaochojoa nguo wakiwa msibani huwa na lengo la kuvutia umati kushiriki mazishi pamoja na kile wanachodai kuwapoza mizimu au kumpa marehemu starehe ya mwisho akielekea katika dunia mpya.

Wanenguaji hawa kwa kawaida ni vijana wadogo wa kike, ambao huimba na kunengua na kuchojoa nguo kuanzia sidiria hadi chupi wakibaki watupu kama walivyozaliwa katika mazishi au misafara ya mazishi.

Kama sehemu ya ibada ya kumombea marehemu, mazishi duniani mara nyingi huhusisha uimbaji na uchezaji kusherehekea tukio hilo, ijapokuwa vitendo vya kuchojoa nguo msibani na mazishini ni vya nadra.

Nchini Taiwan, mila na desturi ilikuwa kuwakodi wataalamu wa kustarehesha mazishi ili kusaidia kusahaulisha familia machungu, hasa wakati ndugu wanaposita au walipopata shida kuhudhuria mazishi.

Madhumuni ya wachojoaji hawa si tu kuvutia umati bali pia kuipoza mizimu inayosumbua pamoja na kufurahisha marehemu mara ya mwisho duniani.

Kinachotokea wakati wa unenguaji kinatofautiana, kinaweza kuhusisha upandaji nguzo na kunengua, mifumo ya sauti, wanamuziki, fataki, taa za rangi zinazobadilika na kila aina ya manjonjo ambayo unaweza kuyakuta katika vilabu vya usiku.

Katika sehemu fulani za vijijini nchini China, kuna makumi ya makundi ya utamaduni ya unenguaji nusu uchi yakitoza yuan 2,000 sawa na Sh 700,000 za Tanzania kwa kila tukio

Wakati mwingine wanenguaji huondoa sidiria au chupi mbele ya vijana wadogo, kitu ambacho kinaweza kusababisha fedheha. Katika baadhi ya tamaduni za Asia hasa Taiwan, kitendo cha unenguaji nusu uchi au watupu kabisa ni kwamba wanafamilia wanataka kuwapo mazishi ya aina yake kuhakikisha marehemu wanasafiri vyema kuelekea dunia mpya.

Mazishi yaliyoandaliwa vyema huvutia watu wengi, kitu wanachohesabu kama alama ya heshima na uletaji wa vikundi vya starehe ni moja ya njia za kufanikisha hilo.

Hata hivyo, kitendo hicho kina utata katika maeneo kama China ambako mamlaka zimechukua hatua za kutaka kukikomesha.

Video za wasichana wakinengua nusu uchi zilizosambazwa katika mitandao kama YouTube, zilisababisha fedheha kwa maofisa wa China hasa wakati zilipoonekana kote duniani.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Utamaduni, serikali imepanga kufanya kazi kwa karibu na polisi kukomesha vikundi vya aina hiyo.

Picha za mazishi katika jiji la Handan katika jimbo la kaskazini la Hebei hivi karibuni zilionesha mnenguaji akiondoa sidiria huku wazazi na watoto wakiangalia. Picha hizo zilisambazwa sana katika mitandao ya jamii na kusababisha kelele.

Katika tukio hilo la Handan, wizara ilisema kwamba wanenguaji sita waliwasili kwa ajili ya kunengua wakiwa nusu uchi katika mazishi ya mkazi mmoja mzee. Wapelelezi walitumwa na kukiri unenguaji huo ulionekana kukiuka sheria za usalama wa umma.

Kutokana na sababu hiyo, mhusika wa kundi hilo alikamatwa na kuswekwa ndani kwa siku 15 na kupigwa faini ya 70,000 sawa na Sh milioni 23.

Serikali ya China imekuwa ikijaribu kukabiliana na wimbi la unenguaji na uchojoaji nguo wakati wa mazishi kwa miaka kadhaa sasa.

Mwaka 2006, kipindi kinachoongoza kwa habari za uchunguzi cha Kituo cha Televisheni cha Central, Jiaodian Fangtan kilirusha kikundi cha wanawake waliokuwa wakinengua na kisha kuchojoa nguo wakati wa ibada ya kumbukumbu ya marehemu katika jiji la Donghai, jimbo la mashariki mwa China la Jiangsu.

Kitendo cha kukodi wachojoaji, ambao wakati mwingine hufanya onesho wakiwa na nyoka huvutia makundi makubwa wakati wa mazishi, bila kufanya hivyo wanakijiji wanakiri usitarajie watu kujitokeza.

Licha ya madai ya mila na desturi, historia ya utamaduni huo nchini Taiwani inaanzia zaidi ya miongo miwili tu iliyopita wakati genge la kimafia la Taiwani lilipohodhi biashara ya mazishi kisiwani humo.

Wakijumuisha na masilahi yao ya kibiashara, waliwakodi wachojoaji kutoka vilabu vya usiku kuwaingiza katika moja ya kampuni zao za uendeshaji wa mazishi.

Ukiritimba wa kifo na ngono upo katika maisha ya kihuni ya genge hilo na kitendo chao kilieneza utamaduni huo hadi ndani ya mipaka ya China wakitumia kisingizio cha mizimu kwa jamii zinazoamini imani za kishirikina.

Hata hivyo, lengo lao kuu lilikuwa kuvutia waombolezaji huku wakidai wachojoaji ni zawadi kwa miungu ambao bado wanafurahia ngono na wanawake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles