Na Samwel Mwanga,
WAZAZI wa wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Maswa wameishauri idara ya elimu kwa kuanzisha kuwapima ujauzito wanafunzi wa kike.
Wanafunzi hao ni kuanzia darasa la tatu hadi kidato cha sita lengo likiwa ni kudhibiti vitendo vilivyokithiri vya wanafunzi hao kupata ujauzito.
Kwa mujibu wa wazazi hao, njia pekee ya kukabiliana na tatizo hilo ni kuanza utaratibu wa kuwapima ujauzito wanafunzi hao wanapokuwapo shuleni.
Walisema miononi mwa matatizo makubwa yanayosababisha kushuka kwa kiwango cha elimu wilayani ni pamoja na wanafunzi wa kike kupatiwa ujauzito wakiwa shuleni na hivyo kukatisha masomo.
“Katika wilaya yetu tuna tatizo kubwa la wanafunzi wetu wa kike hasa wa shule za msingi kutomaliza masomo yao kwa kupatiwa ujauzito.
“Suala hili linachangia kwa kiasi kikubwa kushuka kiwango cha elimu sasa ufike wakati wa kukomesha suala hili,” alisema Angelina Martine.
Walisema dara ya elimu ikishirikiana na idara ya afya wilayani humo iliamua kuchukua hatua hiyo la kudhibiti vitendo vya ngono kwa wanafunzi kwa vile wengi wao ni wenye umri wa kati ya miaka minane hadi 16.
“Unajua wanafunzi wa madarasa hayo wameanza kuwa na umri mkubwa maana ilishawahi kutokea Wilaya ya Bukombe mkoani Geita mwanafunzi wa darasa la tatu akiwa mjamzito.
“Lengo ni kudhibiti vitendo vya ngono kwa wanafunzi shuleni na wakiona upimaji unafanyika wengi wao wataogopa na kujihusisha na vitendo hivyo,” alisema Rhoda John.
Ofisa Elimu Msingi Wilaya ya Maswa,Simon Bujimu, alisema wazo hilo ni zuri na utaratibu huo ulishawahi kutumia na kuwabaini wanafunzi wajawazito.
Alisema kwa sasa zitaongezwa nguvu kupambana na tatizo hilo.
Aliwaomba wazazi nao kukaa chini na watoto wao na kuwaeleza madhara ya kupata ujauzito wakiwa bado masomoni.
Takwimu zinaonyesha katika kipindi cha mwaka mmoja zaidi ya wanafunzi 50 wa kike wa shule za msingi na sekondari wilayani walilazimika kuacha masomo kutokana na ujauzito.