PROFESA KABUDI AONYA VYETI VYA KUZALIWA

0
495

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi, amegeuka mbogo kwa baadhi ya taasisi za Serikali na sekta binafsi zinazokataa kupokea vyeti vya kuzaliwa vilivyoandikwa kwa mkono.

Amesema kwamba, uamuzi huo hauwezi kuvumiliwa kwa kuwa watu wanaoishi vijijini hawawezi kuchapisha vyeti hivyo kwa kuwa mazingira yao hayana kompyuta na vifaa vingine vya kuchapishia nyaraka.

Profesa Kabudi aliyasema hayo wiki iliyopita wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau kuhusu usanifu mpango wa usajili wa matukio muhimu kwa binadamu na ukusanyaji wa takwimu uitwao CRVS.

Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, anazo taarifa za baadhi ya taasisi za Serikali pamoja na sekta binafsi zinazokataa kupokea vyeti kwa sababu vimeandikwa kwa mkono.

Alihoji mtu aliyeko kijijini anawezaje kupata komputa kwa ajili ya kutengeneza cheti hicho na hivyo akawataka wanaohusika kuvipokea mara moja.

“Wanataka vyeti vya komputa, mbona vyeti vya  ndoa na vifo huwa vinaandikwa kwa mkono. Hivi mtu wa kijijini anapata wapi komputa ya kuandikia cheti hicho.

“Kwa hiyo, nawaomba mara moja mvipokee na sitaki tena kusikia malalamiko kuhusiana na kukataa vyeti vinavyoandikwa kwa mkono,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema Serikali ya Tanzania imeamua kufanya maboresho ya mfumo wa usajili uliopo na kuanzisha mfumo utakaofanya kazi vizuri kwa ajili ya usajili wa matukio muhimu ya binadamu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya RITA, Profesa Hamis Dihengo, alisema takwimu za sense ya watu na makazi ya mwaka 2012, zinaonesha asilimia 13.4 ya wananchi ndio wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.

“Pamoja na takwimu hizo, wapo wananchi ambao huzaliwa na kufa bila hata taarifa zao kuonekana katika kumbukumbu zozote za Serikali. Hivyo basi, tunaomba Watanzania wajitokeze kupatiwa vyeti vya kuzaliwa ili Serikali iweze kuwa na takwimu zao,’’alisema Profesa Dihengo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here