BANDARI DAR KUBORESHWA KINA, MLANGO WA KUINGILIA

0
877
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko, akisaini mkataba wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam pamoja na watendaji wakuu wa Kampuni ya China Harbour Engineering na aliyesimama watatu kushoto ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasialiano, Profesa Makame Mbarawa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko, akisaini mkataba wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam pamoja na watendaji wakuu wa Kampuni ya China Harbour Engineering na aliyesimama watatu kushoto ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasialiano, Profesa Makame Mbarawa.

Na KOKU DAVID-DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), hivi karibuni ilitiliana saini na kampuni ya China Harbour Engineering katika Mradi wa Upanuzi na kuongeza Kina cha Bandari ya Dar es Salaam ili kuiongezea uwezo wa kupokea meli kubwa za mizigo pamoja na kushindana na bandari nyingine katika Pwani ya Bahari ya Hindi.

Sambamba na kuiongezea uwezo, pia Serikali imeazimia kuiboresha na kuifanya kuwa yenye miundombinu ya kisasa ambayo itawavutia wafanyabiashara wengi kuitumia kupitisha mizigo yao.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ambaye alikuwa shuhuda wakati wa kutiliana saini hizo, anasema Serikali imeamua kutanua Bandari ya Dar es Salaam ili kuiwezesha kubeba mizigo mingi na pia itaboresha miundombinu yake.

Anasema mradi huo ambao utagharimu Sh bilioni 336 utaanza baada ya Rais John Magufuli kuweka jiwe la msingi mwanzoni mwa Julai na kwamba utakamilika baada ya miezi 36 ambapo utahusisha uongezaji wa kina cha lango la bandari pamoja na uongezaji wa kina cha maji kati ya gati namba 0, moja hadi saba.

Anasema kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam haina uwezo wa kubeba meli kubwa za kimataifa kutokana na kuwa kina cha maji kilichopo ni kifupi, ikiwa ni pamoja na miundombinu isiyoendana na wakati.

Anasema kina cha maji katika gati namba 0 kitajengwa upya na kitakuwa ikitumika kushushia magari na kwamba kina cha maji kuanzia gati namba moja hadi saba kitaongezwa urefu na kufikia mita 15 kila moja kutoka mita nane iliyopo sasa.

“Upanuzi huu unalenga kuifufua upya Bandari ya Dar es Salaam ili iweze kufanya kazi kwa ushindani, kuhudumia wateja wengi, kupokea meli kubwa na za kisasa zenye uwezo wa kubeba makontena 19,000, ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi na kukuza uchumi wa nchi.

“Katika gati namba nane, kina chake cha maji kina urefu wa mita 10.5 hadi 11 wakati kina kinachotakiwa ni mita 12 hadi 13, hivyo ili kuifanya bandari yetu kuwa na ushindani mkubwa tutarefusha kina katika kila gati hadi kufikia urefu wa mita 15 pamoja na kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa, barabara pamoja na kuweka mashine zitakazoweza kupakuwa mizigo kwa muda mfupi.

“Pesa za ujenzi wa mradi huu zimetokana na mkopo wa masharti nafuu wa dola milioni 345 ambazo Serikali imekopeshwa na Benki ya Dunia na kwamba tunatarajia ujenzi huu utakamilika kwa muda uliopangwa,” anasema Profesa Mbawara.

Anasema baada ya kukamilika kwa upanuzi huo wa bandari pamoja na reli ya kisasa, wanaamini bandari hiyo itakuwa kivutio hasa ikizingatiwa kuwa katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/18 tozo ya kodi katika usafirishaji mizigo imeondolewa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko, anasema mradi huo utakapokamilika wanatarajia ongezeko la mizigo kutoka tani milioni 14 hadi 28 ifikapo mwaka 2022.

Anasema kwa sasa bandari hiyo hupokea meli 30 hadi 40 za mwambao na za kimataifa, lakini takribani meli nane hadi 10 husubiria nje kutokana na kina cha mita 10.5 hadi 11 kilichopo bandarini hapo ambacho hakina uwezo wa kupokea meli nyingi na kubwa.

Anasema kutokana na upanuzi huo kwa gati zilizokusudiwa, Bandari ya Dar es Salaam itawezesha kupokea meli kubwa zenye uwezo wa kubeba kontena 8000 hadi kufikia 10,000 hapo baadaye.

“Mradi huu utakapokamilika tutaweza kupokea meli kutoka katika nchi tunazofanya nazo biashara kama China, Uingereza, Japani, Marekani na Ulaya kuja moja kwa moja katika bandari yetu na hicho ndicho kilichokuwa kilio chetu.

“Mpaka mradi wote unakamilika tutakuwa na gati nane zenye vina vya maji vitakavyomudu kubeba meli kubwa na baadaye tutaongeza hadi gati namba 15, lakini pia tuna makusudio ya kujenga na ule upande wa pili katika mradi huo huo ambao unaweza kutuchukua labda mpaka mwaka 2023,” anasema Kakoko.

Anasema upanuzi huo utaifanya bandari hiyo kurejesha heshima yake na kwamba iwapo isipojengwa kwa kiwango cha kisasa, ifikapo 2020 mizigo ambayo inaweza kupokewa ni milioni 20 tu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya China Harbour Engineering, Xu Xinpei, anasema baada ya makubaliano hayo wanatarajia kuijenga bandari hiyo katika viwango vya juu na kuifanya kuwa ya kwanza kwa ubora na itakayotoa huduma nzuri Afrika Mashariki.

Anasema pia wanatarajia kuikamilisha ndani ya muda na wakati uliokubaliwa, ikiwa na viwango vinavyostahili.

Kwa upande wake, Meneja Masoko wa Shirika la Reli Tazara, Everist Kasumbai, anasema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa Taifa kutokana na kutakuwa na ongezeko la mizigo kutoka ndani na nje ya nchi.

Anasema kwa upande wa shirika la reli, hivi sasa hali imeanza kuimarika kutokana na ongezeko la mizigo kutoka Congo, Malawi na Zambia na kwamba wanajipanga kuhakikisha wanashirikiana na Bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

“Hivi sasa tunapata msaada kutoka Serikali zetu mbili za Tanzania na Zambia na kwamba baada  ya hili suala la VAT kuondolewa tunaamini wateja wetu kutoka Congo, Malawi na Zambia watarudi kutumia  Bandari ya Dar es Salaam, hali itakayowezesha kupokea mizigo mingi,” anasema Kasumbai.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here