24 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi St. Joseph waishitaki TCU kwa Waziri wa Elimu

Pg 3Na Grace Shitundu, Dar es Salaam

WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph kilichopo Mbezi Luguruni, Dar es Salaam, wameishtaki  Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kwa kushindwa kutatua changamoto zao kwa wakati.

Waziri Profesa Ndalichako alifika chuoni hapo jana asubuhi kwa lengo la kuwasikiliza wanafunzi hao ambao walikuwa na mgomo kwa siku tatu mfululizo, wakishinikiza Serikali  kuingilia kati na kutatua matatizo yao ambayo wanadai yamekuwapo tangu mwaka 2013.

Profesa Ndalichako aliwasili chuoni hapo saa 3 asubuhi  na kufanya mazungumzo na uongozi wa chuo, serikali ya wanafunzi na baadae wanafunzi wote.

Wanafunzi hao, walimwambia Profesa Ndalichako kuwa TCU na uongozi wake ni jipu linalotakiwa kutumbuliwa.

Waziri huyo alikutana na wanafunzi wote ambao walimpokea kwa sauti kubwa wakiimba “TCU jipu”, ambapo hata hivyo aliwapoza na kuwaambia kilio chao amekisikia.

Waziri wa Elimu wa Serikali ya chuo hicho, Emmanuel Lyatuu alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakifuatilia utatuzi wa changamoto zinazowakabili, lakini wamekuwa wakipata majibu yasiyoridhisha kutoka kwa Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya.

“Mpaka tumefikia hatua ya kuhitaji kukutana na wewe, ni kutokana na majibu tunayopata kutoka kwa Profesa Mgaya hayaridhishi,” alisema.

Kwa upande wake Rais wa Serikali ya Wanafunzi, Celestine Makota, alisema wanafunzi hao wanakabiliwa na matatizo mengi ambayo kwa muda mrefu yamekosa majibu.

Alisema  chuo hicho hakina ubora wa kutoa mafunzo ya uhandisi na kozi nyingine kutokana na kutokuwa na walimu wa kutosha wenye sifa na wengi wao ni raia kutoka India.

“Chuo hakina qualified lecturers wa kutosha hasa seneior Lecturers, hakuna profesa hata mmoja, huku madaktari wa PHD hawazidi hata wanne ambao wamebobea kwenye masomo ya kompyuta,  engeneering (uhandisi) au communications (mawasiliano) na badhi ya kozi hazina wahadhiri kabisa.

“Workshops na Labs ni chache, ndogo na hazina vifaa vya kutosheleza, maktaba iliyopo ina vitabu vichache na vile  muhimu havipo.

“Ada nayo ni tatizo jingine, hailingani na huduma ya masomo  tunayopata katika chuo hiki. Pia kumekuwa na ucheleweshaji wa fedha za chakula na masomo.

“Jingine ni kuhusu vyeti huwa vinachelewa kutoka, pia kuna wenzetu ambao wamemaliza wanalalamika kutopokelewa ‘field’ kwa kuwa hatutambuliki,” alisema Makota.

Kutokana na matatizo hayo Waziri Ndalichako aliitaka TCU kupitia upya sifa za walimu wanaofundisha katika chuo hicho na pia kuutaka uongozi wa chuo hicho kurekebisha kasoro zilizopo haraka iwezekanavyo.

“Nawaagiza TCU kupitia upya na kuangalia sifa za walimu kama wanafaa na pia matatizo mengine ambayo mengi ni ya kiutawala hivyo uongozi wa chuo uyafanyie kazi mapema ili wanafunzi wanapofungua chuo wakute yamekwisha” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles