27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Ajali ya daladala yaua wanne Dar

ajali-3Veronica Romwald na Asifiwe George, Dar es Salaam

VILIO na simanzi jana vilitawala eneo la Tabata Matumbi, Dar es Salaam, baada ya basi la abiria linalofanya safari zake kati ya Gongo la Mboto na Kituo cha  Simu 2000 lenye namba za usajili T 629 CTT kugongana na magari mawili na kusababisha vifo vya watu watatu papo hapo.

Ajali hiyo ilitokea barabara ya Mandela saa 11 alfajiri, ikihusisha pia lori lenye namba za usajili T 447 DBH na gari jingine aina ya Scania lenya namba za usajili T 109 DDX.

MTANZANIA lilifika eneo la tukio na kukuta umati wa watu waliokuwa wakishangaa tukio hilo, huku wakiwa na nyuso za huzuni.

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Mwanaidi Seif alisema alishuhudia namna magari hayo yalivyogongana yakiwa katika mwendo wa kasi.

“Ajali hii ni mbaya mno… sijawahi kuona maishani mwangu damu imemwagika kama tupo machinjioni… binafsi kabla haijatokea nilishuhudia magari haya hasa lile la abiria, dereva alikuwa  mwendo wa kasi, ukiliangalia lile basi limevunjika lote utafikiri ni chuma chakavu,” alisema.

Alisema ghafla alishuhudia lori la mchanga lililokuwa likiendeshwa kwa mwendo kasi, likigonga basi la abiria na kupoteza mwelekeo.

“Kwa kuwa dereva wa gari la abiria alikuwa mwendo kasi, alishindwa kulimudu na kujikuta likihamia upande wa pili wa barabara ambako huko alikwenda kugongana na lori jingine,” alisema Mwanaidi.

Naye Salum Karim, alisema alishuhudia ajali hiyo, huku watu wengi wakijeruhiwa na wengine wakipoteza maisha.

“Watu wengi waliumia sehemu mbalimbali za miili yao na kuna gari lilifika likawachukua majeruhi na wale waliofariki dunia kuwakimbiza hospitali.

“Mbali na watu  kuumia na wengine kupoteza maisha, pia kuna baadhi ya ng’ombe ambazo walikuwa wamepakiwa kwenye lori upande wa pili walikufa,” alisema.

Wapelekwa Amana

Majeruhi wote, walipelekwa Hospitali ya Amana kwa ajili ya matibabu, huku miili ya marehemu ikihifadhiwa kwa ajili ya kusubiri taratibu za kutambuliwa na ndugu zao.

Akizungumza na MTANZANIA ofisini wake, Daktari Kiongozi wa Hospitali ya Amana, Stanley Dinagi alisema walipokea majeruhi 26 na miili ya watu watatu.

“Walianza kuletwa hapa saa 12 asubuhi, tulipokea majeruhi 26 na miili mitatu ya watu walipoteza maisha palepale katika eneo la ajali. Tulianza kuwahudumia majeruhi, baadae mmoja wao alifariki dunia, wakabaki  25,” alisema.

Alisema miongoni mwa majeruhi hao, wapo wanawake tisa na wanaume 16 na mtoto mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja.

Alisema majeruhi watano ambao hali zao ni mbaya, walihamishiwa  Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi.

“Wengi wao wana michubuko na wapo waliochanika sehemu mbalimbali za miili yao, tumewafanyia kipimo cha X-ray na wengine tumewafunga ‘POP’. Wapo walioumia sehemu za kichwani  tumelazimika kuwahamishia Muhimbili ili wakachunguzwe kwa kipimo cha CT-Scan,” alisema Dk Dinagi.

Dk.Dinagi alitaja majeruhi waliolazwa, kuwa ni Venance Iliaeli (17), Wilence Lymo (28), Deo Kimario (19), Gasper John (25), Yasin Abdalah (25), Abbas Nassoro (38) wote wakazi wa Gongo la Mboto.

Wengine, ni Amina Ridhiwani (19) mkazi wa Buza, Samiat Salim (23) mkazi wa Tabata, Rozalia Malawaiya (22) Chang’ombe, Jummanne Simon (23) mkazi wa wa Yombo Relini na Stephano Tibu (34) mkazi wa Banana.

“Wengine ni Didas Lucas (39) mkazi  wa Banana, Said Hussein (35) mkazi wa Kitunda,Salim Basher (27) mkazi wa Ukonga, Hussein Yunus (1) mkazi wa Kiteto mkoani Manyara na Mwanaisha Ramadhani (43) mkazi wa Buguruni,” alisema.

Dk. Dinagi, ametoa wito kwa wananchi kufika hospitalini hapo ili kutambua miili ya marehemu.

“Hadi sasa tumetambua jina la marehemu mmoja ambaye anaitwa Godfrey Nyamwenga… huyu alikuwa na kitambulisho mfukoni, wengine hatujawatambua, tunawaomba wananchi waje kutambua miili tuliyohifadhi,” alisema.

Majeruhi anena

Akizungumza na MTANZANIA mmoja wa majeruhi aliyelazwa hospitalini hapo, Jeni Ngama, mkazi wa Gongo la Mboto alisema anamshukuru Mungu kwa kumwokoa.

“Ajali ile ilikuwa mbaya kwa kweli, nakumbuka ilikuwa saa 11 hivi, tulikuwa tunatoka Gongo la Mboto kuelekea Ubungo, tulipofika Buguruni Sheli dereva aliingia kituoni na kushusha abiria kadhaa.

“Tulipotoka pale, dereva aliondoka kwa mwendo wa kasi kidogo, baadae nilishangaa kuona lori limetokea kwa mbele yetu, yeye alijitahidi kulikwepa na kuingia upande wa ‘service road,’ ghafla nikashangaa tumepata ajali ile,” alisema mama huyo huku akiugulia maumivu.

“Nahisi maumivu mno, nitapelekwa Muhimbili kwa vipimo zaidi, nawasihi madereva wawe makini na kuepuka kuendesha kwa mwendo kasi maana watatumaliza,” alitoa rai.

Muhimbili

Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, Neema Mwangomo alisema hadi kufikia saa saba mchana, walikuwa wamepokea majeruhi wanne waliopewa rufaa kutoka Hospitali ya Amana.

“Majeruhi hao, ni Victoria Msangi (21)  mkazi wa Tabata, Janeth Mwakyusa (18) wa Ukonga, Bakari Jafari (26) mkazi wa  wa Mbagala, Neema Kimario (34) na Rabia Omari (37) wakazi wa Gongo la Mboto,” alisema.

Kauli ya Kamanda

Naye Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama barabarani,  Mohamed  Mpinga alisema lori lililokuwa limebeba mchanga, lilikuwa linaenda mwendo kasi hivyo liligonga basi la abiria ambalo lilihamia  upande wa pili kisha kugongwa na lori lililokuwa limebeba ng’ombe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles