ALLAN VICENT-TABORA
Wanafunzi wa Chuo cha Musoma Utalii Mkoani Tabora wamepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano katika kuboresha elimu nchini ikiwemo kuondoa ada na michanga yoyote.
Wakizungumza na gazeti hili wanafunzi hao wamesema kuwa uamuzi wa serikali wa kuondoa ada na michango yote kuanzia shule za awali, msingi hadi sekondari umetoa fursa kubwa sana kwa watoto wengi kupata elimu na kujiunga na vyuo.
Wamesema kuwa hatua hiyo imeondoa dhana ya baadhi ya wanafunzi waliokuwa wakianza shule na kuishia njiani kutokana na uwezo duni wa wazazi wao huku wakijifariji kuwa angalau wamefuta ujinga japo kwa kujua kusoma na kuandika tu.
Mwanafunzi wa taaluma ya uandishi wa habari na utangazaji katika chuo hicho Alfonse Lwiza (22) amesema kuwa serikali imefanya jambo la maana sana kuondoa ada na michango yote shuleni kwani kwa kufanya hivyo itahamasisha wanafunzi wengi zaidi kusoma na hatimaye kujiunga na vyuo.
Kwaupande wake Mkurugenzi wa Chuo hicho Shaaban Mrutu amesema kuwa Chuo chake kinaunga mkono jitihada zote zinazofanywa na serikali katika kuboresha suala la elimu huku akisisitiza kuwa elimu inayotolewa chuoni hapo inakidhi vigezo vyote vya soko la ajira.