ALLAN VICENT-TABORA
Kampeni ya ukusanyaji chupa za plastiki zilizozagaa mitaani iliyoanzishwa na Kampuni ya Cocacola inatarajiwa kuzinufaisha shule za sekondari hapa nchini zitakazokusanya chupa nyingi zaidi kuliko nyingine.
Hayo yamebainishwa leo Jumanne Mei 21 na Meneja Mauzo na Masoko wa Kampuni ya Nyanza Bottlers ambayo ni Kampuni dada wa Coca cola Samwel Makenge, katika hafla ya kutambulisha kampeni hiyo mkoani Tabora.
Amesema kuwa kampeni hiyo iliyozinduliwa wiki iliyopita na kupewa jina la ‘Rejesha na Ushinde’ imelenga kuleta mabadiliko ya kudumu ya utunzaji mazingira katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Amebainisha kuwa wahusika wa kampeni hiyo ni shule zote za sekondari hapa nchini na wanafunzi watatakiwa kuokota chupa nyingi kadri wawezavyo na kuzitunza shuleni kwao na shule itakayokusanya chupa nyingi zaidi itapata zawadi.
‘Shule zitakazofanya vizuri sana katika kampeni hii zitajipatia zawadi mbalimbali zilizoandaliwa na Kampuni ya Coca cola ikiwemo kuboreshwa kwa uwanja wa mpira wa miguu wa shule itakayoshika nafasi ya kwanza’, amesema Makenge.
Makenge ametaja zawadi nyingine kuwa ni pamoja na mashine ya kudurufu (photocopier), projekta 2, komputa mpakato 108, komputa 11, vishikwambi (tablets) 108, saa 12, jezi 1176 na mipira 360 kwa washindi wa kila kipengele.