21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi Bwawani wanolewa kielimu, ujasiriamali

Na Ashura Kazinja, Morogoro

KATIKA kukabiliana na changamoto ya ajira na uharibifu wa mazingira nchini shule ya Sekondari Bwawani iliyoko mkoani Pwani imeamua kutumia nishati ya gesi kupikia, kupanda miti, ufugaji pamoja na kuanzisha kiwanda kidogo cha kutengenezea mikate.

Wanafunzi shule ya sekondari Bwawani wakiimba katika mahafali ya kuwaaga wahitimu wa kidato cha sita shuleni hapo.

Akizungumza katika mahafali ya saba ya kidato cha sita yaliyofanyika shuleni hapo juzi, Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Bwawani iliyopo mkoa wa Pwani katika Halmashauri ya Chalinze, Anthon Sogoseye, amesema kuwa wanatunza mazingira kwa kupanda miti na kutumia gesi kupikia chakula cha wanafunzi hali iliyopelekea kuboresha chakula pamoja na kupunguza uchafu wa mazingira.

Mwalimu Sogoseye amesema katika jitihada za kutunza mazingira shule hiyo imeamua kutumia nishati ya gesi kwa ajili ya kupikia badala ya kuni au mkaa na hivyo kuokoa miti mingi ambayo ilikuwa inatumika kama kuni na kutunza mazingira sambamba na kuokoa muda mwingi uliokuwa unatumika kutafuta kuni na hata kupika chakula.

“Pamoja na kushiriki masomo ya darasani, wahitimu wameshiriki katika kutunza mazingira kwa kupanda miti ya kivuli na matunda kupitia vikundi vyao vya ‘Mali hai’ na ‘Skauti’ pamoja na matumizi ya gesi ambayo imeboresha ubora wa chakula shuleni hapo,” amesema Sogoseye.

Akizungumzia changamoto zinazoikabili shule hiyo amesema nipamoja na baadhi ya wazazi na walezi kutolipa ada kikamilifu na kwa wakati, hali inayosababisha baadhi ya wanafunzi kukatisha masomo yao na kurudi nyumbani kufuata ada na hivyo kuwaathiri wanafunzi hao kitaaluma na wakati mwingine kisaikolojia.

Kwa upande wake Kamishna wa Utawala na Rasilimali watu wa Jeshi la Magereza, DCP Jeremiah Katungu, ambae alikuwa ni mgeni rasmi alisema amefurahishwa na kukamilika kwa miradi mbalimbali shuleni hapo, ambayo kwa kiasi kikubwa imechangia kuboresha maendeleo ya kitaaluma, kwani   taaluma inategemea sana uwepo wa miundombinu ya msingi kama madarasa, maabara, maktaba pamoja na ubora wa afya ya mwanafunzi mwenyewe.

Vilevile aliwataka wanafunzi wahitimu na wanaoendelea na masomo kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya shule hiyo ‘Nidhamu, elimu na fadhila’ ili taifa liweze kupata viongozi bora wenye uadilifu na wazalendo, na kuwataka wazazi, walimu na wanafunzi kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili shuleni hapo.

“Nadhani wote ni mashahidi au mmepata kusikia kupitia vyombo vya habari jinsi baadhi ya watumishi wasivyo waadilifu katika taifa letu ambao wameshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo,” alieleza DCP Katungu.

Hata hivyo, ameitaka jamii kwa ujumla kubadili tabia zinazoweza kuchangia maambukizi ya ukimwi na mimba za utotoni, kwani wengi wanaoathirika na ugonjwa huo na wanaopata mimba ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya kujenga taifa, na watoto wa kike ndio waathirika wakubwa.

Nao wahitimu wa kidato cha sita, John Msami na Irine Mkwawa, wakisoma risala kwa mgeni rasmi waliupongeza uongozi wa shule hiyo kwa kufanya ukarabati wa mabweni, ujenzi wa kiwanda kidogo cha mikate pamoja na matumizi ya gesi katika jiko la kupikia chakula cha wanafunzi.

Nae mwanafunzi wa kidato cha sita Shabani Ayubu alisema mbali na masomo pia wanajifunza ujasiliamali kwa kujifunza ufugaji na namna ya kutengeneza mikate, kazi itakayowasaidia kujiajiri na kuacha kutegemea kuajiriwa watakapohitimu masomo yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles