
Na RAMADHAN HASSAN, DODOMA
SERIKALI imetangaza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2017, huku 28,638 wakikosa nafasi za kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na sababu mbalimbali.
Matokeo hayo yalitangazwa mjini hapa jana na Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa Simbachawene, kati ya wanafunzi 526,653 waliochaguliwa, 28,638 wamekosa nafasi katika awamu ya kwanza.
“Kati ya hao, wavulana ni 12,937 na wasichana 15,701. Katika hili, Mkoa wa Dar es Salaam ndio unaoongoza kwa kuwa na wanafunzi 18,820 waliokosa nafasi katika awamu ya kwanza,” alisema Simbachawene.
18,000 WAKOSA NAFASI DAR
Wanafunzi 18,820 kati ya 51,488 waliofaulu mtihani wa darasa la saba Mkoa wa Dar es Salaam wamekosa nafasi za kujiunga kidato cha kwanza mwakani. Waliochaguliwa kujiunga ni 32,668.
Hayo yalibainishwa na Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Theresia Mmbando, baada ya kikao cha uchambuzi wa wanafunzi hao baina yake na maofisa elimu wa wilaya na mkoa.
Katika hatua nyingine, Mmbando aliipongeza Shule ya Msingi Tusiime kwa wanafunzi wake kufanya vizuri na kuongoza katika kumi bora kwa upande wa wavulana na wasichana.