25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Godbless Lema bado mambo magumu

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), akiwa chini ya ulinzi wakati akielekea kupanda gari kupelekwa gerezani, baada ya rufaa yake ya maombi ya dhamana kushindwa kusikilizwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha jana.
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), akiwa chini ya ulinzi wakati akielekea kupanda gari kupelekwa gerezani, baada ya rufaa yake ya maombi ya dhamana kushindwa kusikilizwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha jana.

Na JANETH MUSHI, ARUSHA

MAWAKILI wa Serikali, Matenus Marandu na Paul Kadushi, wameweka pingamizi la awali katika Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, wakiiomba isisikikize maombi ya rufaa juu ya dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), yaliyokuwa yasikilizwe jana.

Kutokana na pingamizi hilo, Lema alirudishwa mahabusu hadi Desemba 2 mwaka huu, rufaa yake itakaposikilizwa.

Pamoja na pingamizi hilo, jana saa 3:20 asubuhi, mawakili wa Lema na Serikali walikutana katika chumba cha ofisi ya Jaji Mfawidhi, Fatuma Masengi, ambaye alikuwa asikilize rufaa hiyo.

Baadaye Wakili Marandu aliwaeleza waandishi wa habari kwamba wameweka pingamizi hilo kwa kuwa mawakili wa Lema hawakuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa na badala yake walikata rufaa moja kwa moja.

“Tumeweka pingamizi hilo chini ya kifungu cha 361(1) (a) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

“Baada ya mjadala, tumekubaliana kwa pamoja kuharakisha pingamizi hilo na kuamua lisikilizwe kwa njia ya maandishi, na upande wa Serikali utawasilisha hoja zake Novemba 30, mwaka huu, saa mbili asubuhi, na upande wa utetezi siku hiyo hiyo watajibu hoja hizo saa sita mchana, na hoja za nyongeza tutawasilisha saa tisa alasiri,” alisema Wakili Marandu.

Rufaa hiyo ilikatwa Novemba 22, mwaka huu, chini ya hati ya dharura na mawakili wa mbunge huyo, Peter Kibatala, Adam Jabir, Sheck Mfinanga na Faraji Mangula.

Katika rufaa hiyo, mawakili hao wanadai haki ya dhamana ya Lema aliyonyimwa kutokana na makosa ya kisheria yaliyofanywa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Novemba 8, mwaka huu.

Wakati wakili huyo akisema hayo, Wakili Kibatala alidai kuwa walipokea pingamizi hilo la mawakili wa Serikali jana saa 3:15 asubuhi.

“Kama Jaji Masengi atatupilia mbali pingamizi hilo, rufaa yetu itaweza kusikilizwa na uamuzi utatolewa Desemba mbili, mwaka huu, saa tatu asubuhi,” alisema.

Rufaa hiyo ilipokewa mahakamani hapo hivi karibuni na kusajiliwa kwa namba 112 na 113 ya mwaka 2016.

Mawakili wa Lema wanadai kuwa Hakimu Desideri Kamugisha, wakati anasikiliza shauri hilo, alisema mahakama hiyo ingempa Lema dhamana kwa masharti itakayoweka.

Lakini kabla hajamalizia kutoa uamuzi wake, mawakili wa Serikali walisema wameandaa notisi ya rufaa juu ya uamuzi huo na hoja hiyo ikaridhiwa na hakimu huyo.

Kwa mujibu wa mawakili wa Lema, kilichofanywa na Hakimu Kamugisha ni makosa ya kisheria, kwa mahakama kukubali maombi ya mawakili wa Serikali kabla mahakama haijamaliza kutoa uamuzi wake.

Kutokana na uamuzi huo, Lema kupitia kwa mawakili wake, waliandika barua ya maombi kuiomba Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha kufanya marejeo ya mwenendo wa kesi za jinai zinazomkabili mtuhumiwa huyo katika mahakama ya chini, lakini mawakili hao wa Serikali waliweka pingamizi ili Mahakama Kuu isisikilize maombi hayo.

Lema ambaye ana siku ya 26 tangu alipokamatwa Novemba 2, mwaka huu nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma, hadi sasa yuko katika Gereza la Kisongo, mjini hapa akikabiliwa na kesi za jinai namba 440 na 441.

Katika kesi hizo, anatuhumiwa kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli kupitia mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali jijini hapa.

Wakati huo huo, askari magereza waliokuwa mahakamani hapo jana, waliendelea na misuguano na waandishi wa habari baada ya kuwatuhumu kuwa walitaka kuwanyang’anya bunduki zao.

Kutokana na hali hiyo, askari hao waliwakamata waandishi Theodora Mrema (Star TV) na Lucas Myovela wa Sunrise Radio ya jijini hapa.

Katika hatua nyingine, Lema anaweza akaendelea kusota gerezani kama maombi ya rufaa yake ya dhamana hayatasikilizwa na kupata dhamana ifikapo Desemba 15, mwaka huu.

Hali hiyo inatokana na taarifa kutoka vyanzo vya kuaminika zinazoonyesha kuwa majaji wa mahakama hiyo, wanatarajia kuanza likizo.

Kama hilo litatokea, Lema atalazimika kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya wa 2017, akiwa gerezani Kisongo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles