27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

WANAFUNZI 28,000 WAKOSA NAFASI SEKONDARI

JONAS MUSHI NA CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM


 

wanafunziWANAFUNZI 28,638 wamekosa nafasi ya kujiunga na sekondari mwakani kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Licha ya Serikali kufanya jitihada za kuhakikisha inatokomeza kabisa uhaba wa madawati shuleni, sasa changamoto imekuwa ni madarasa na kusababisha wanafunzi kusomea nje katika baadhi ya shule.

Takwimu zinaonyesha karibu nusu ya wanafunzi wanaoandikishwa darasa la kwanza hawahitimu darasa la saba na wanaobakia shuleni hawatoshelezwi na miundombinu iliyopo.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Takwimu za Taifa za Elimu ya Msingi (BEST) ya mwaka 2006-2010, wanafunzi 1,356,574 waliandikishwa darasa la kwanza mwaka 2010, lakini waliofika na kuhitimu darasa la saba mwaka 2016 kwa mujibu wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), ni 795,739 sawa na asilimia 58.6 ya walioandikishwa darasa la kwanza.

Hali hiyo ndiyo iliyojitokeza kwa upande wa sekondari ambapo kwa kidato cha kwanza pekee, zaidi ya wanafunzi 28,000 wanakosa nafasi.

Kwa mujibu wa Mtandao wa Takwimu Huria za Taifa zilizochapishwa 2015, zinaonyesha kuna jumla ya madarasa ya shule za sekondari za Serikali 52,404 nchi nzima na wanafunzi 1, 580,810, ikiwa na uwiano wa darasa moja kwa wanafunzi 30.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwanzoni mwa wiki hii na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, mikoa ambayo wanafunzi wamekosa nafasi kwa awamu ya kwanza na idadi yao kwenye mabano ni Dar es Salaam (18,820), Arusha (4,752), Songwe (1,465), Kigoma (1,208), Manyara (1,141), Lindi (608), Mbeya (406) na Katavi (238).

Serikali ilitangaza wanafunzi 526,653 sawa na asilimia 94.8 ya waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka huu na wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani katika shule za sekondari za serikali katika awamu ya kwanza.

Katika Manispaa ya Ilala Dar es Salaam, kuna upungufu wa madawati 7,820 na vyumba 357 vya madarasa kwa shule za sekondari.

Katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Manispaa imepanga kujenga vyumba 39 tu vya shule ya sekondari ambavyo vitagharimu Sh bilioni 1.9, hivyo inaonyesha kutaendelea kuwa na upungufu wa madarasa 318 hadi mwaka huu wa fedha unaisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles