25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

WANA CCM WAZUIWA KUMWONA MAGUFULI

Na GUSTAPHU HAULE – PWANI


magufuli-610x415ZAIDI ya wanachama 100 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Halmashauri ya Kibaha Mjini, Mkoa wa Pwani, wamezuiwa kuingia katika viwanja vya mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OCCM), yaliyofanyika jana eneo la Bungo, wilayani Kibaha.

Tukio hilo lilitokea baada ya wana CCM hao kudaiwa kuwa hawakuwa na vitambulisho vya kuingilia katika mahafali hayo ambayo mgeni rasmi alikuwa Rais Dk. John Magufuli.

Pamoja na Rais Magufuli, alikuwapo pia Mkuu wa chuo hicho, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu wa CCM, Kata ya Mailimoja, Maulid Mkwike, alisema alipata taarifa ya ujio wa Rais katika mahafali hayo juzi na kulazimika kuwajulisha wana CCM wenzake.

“Kwa hiyo, leo (jana) saa tatu asubuhi nikiwa na wana CCM wenzangu, tulikwenda katika mahafali hayo, lakini tulizuiwa kuingia getini kwa sababu hatukuwa na mwaliko.

“Wakati huo tulikuwa tumevaa sare zetu za chama, lakini tulipofika pale getini, tuliambiwa tutoe vitambulisho vya mwaliko, lakini hatukuwa navyo,” alisema Mkwike.

Akizungmzia tukio hilo, aliyekuwa mgombea udiwani Kata ya Mailimoja wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, Christopher Mjema, alisema kuwa walikwenda katika mahafali hayo kumwona Rais Magufuli kwa kuwa ni kiongozi mkuu wa chama chao.

“Magufuli ni kiongozi wetu, kwa hiyo, tulikwenda katika mahafali hayo kuonana naye. Pamoja na kwamba tulizuiwa kuingia, umefika wakati sasa uwepo utaratibu maalumu wa viongozi wa chama na hata wa Serikali, kuhudhuria katika hafla zinazofanyika katika maeneo fulani fulani,” alisema Mjema.

Naye Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Kibaha Mjini, Maulid Bundala, alisema anasikitishwa na tukio la kuzuiwa kuingia katika mahafali hayo.

Wakati huo huo, Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM Taifa, imeridhishwa na juhudi na mikakati inayoendelea kuelekea jumuiya hiyo kujitegemea kiuchumi kwa asilimia 100.

Kamati hiyo imefikia uamuzi huo katika kikao cha kamati hiyo kilichokaa hivi karibuni chini ya Mwenyekiti wake Sadifa Juma Khamisi katika ukumbi wa mikutano Makao Makuu ya UVCCM, Dar es Salaam.

“Ili kuweza kujiendesha kwa ufanisi na mafanikio, kamati imeridhia uondoshwaji wa wafanyabiashara wote waliopo eneo la UVCCM  Kinondoni Mwinjuma ili kupisha uvunjaji na hatimaye kuanza kwa ujenzi wa vitega uchumi vikubwa katika eneo hilo.

“Wafanyabiashara waliopo watapewa notisi ya siku 90 ili wawe wameondoka katika eneo hilo. Uwekezaji mpya katika eneo hilo takriban kwa asilimia 99 utagharimiwa na UVCCM yenyewe,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema kuwa kufuatia tathmini iliyofanywa na UVCCM Taifa nchi nzima kwa kutathmini miradi yake kuanzia ngazi ya shina hadi taifa,  kamati imeamua na kuelekeza kuimarishwa mfumo wa ukusanyaji mapato wa jumuiya na kusimamia matumizi yake sambamba na kupitia upya mikataba yote ya uwekezaji.

Ilisema kuwa kamati ya utekelezaji imeziagiza wilaya na mikoa kutambua kuwa mali na rasilimali za jumuiya si milki ya mtu au kiongozi, kila aina ya mali au kitega Uchumi cha Jumuiya, kinahitaji kulindwa, kutunzwa na kuhifadhiwa na wanajumuiya wote hivyo imewakumbusha kuanzia sasa ni lazima kutekeleza Azimio la Siasa na Uchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles