ELIZABETH HOMBO Na ANDREW MSECHU
-DAR ES SALAAM
UTAFITI wa Taasisi ya Twaweza umeonyesha umaarufu wa Rais Dk. John Magufuli umeshuka kutoka asilimia 96 mwaka 2016 hadi 55 mwaka huu, huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikipoteza umaarufu wake maeneo ya vijijini.
Matokeo ya utafiti huo yaliyotolewa jana Dar es Salaam, yanaonyesha pia umaarufu wa wabunge, madiwani umeshuka.
Utafiti huo pia umeonyesha uungwaji mkono wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) umeshuka kutoka asilimia 25 mwaka 2015 hadi 16 mwaka huu.
Vilevile idadi kubwa inaongezeka ya wananchi ambao hawako karibu na chama chochote cha siasa kutoka asilimia 17 mwaka 2017 hadi 24 mwaka huu.
Katibu Mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole, miongoni mwa wadau waliohudhuria kikao cha kutangaza matokeo hayo, alisema suala la kushuka kwa umaarufu wa Rais, ni la muda na kuwa kazi ya maendeleo inayofanywa na Serikali italeta matunda mbeleni na umaarufu wake utarudi juu.