29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, October 2, 2022

KANGI LUNOLA AFUTA BARAZA LA USALAMA BARABARANI

 

Na PENDO FUNDISHA-MBEYA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amevunja Baraza la Taifa la Usalama Barabarani.

Vilevile  amezivunja  kamati za baraza hilo za mikoa na wilaya nchini hadi litakapoundwa upya na kutangazwa kwa maslahi ya taifa.

Kangi alichukua hatua hiyo jana mjini hapa baada ya kusema amejiridhisha kwamba baraza hilo limeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na malengo ya kuanzishwa kwake.

Alikuwa akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Baraza la Usalama Mkoa wa Mbeya.

Kangi alisema haiwezekani baraza likaongozwa na viongozi ambao hawajielewi wala kutambua majukumu yao.

Alisema  ni bora lisiwepo kwa muda hadi  wizara yake itakapounda baraza jipya litakalosaidia kupambana na ajali za barabarani.

“Nimekutana na baraza la usalama barabarani la Mkoa wa Mbeya, nikamuuliza mwenyekiti majukumu yake, lakini  hakuna anachoelewa wala anachokifahamu.

“Nikamuuliza kamati yake ina watu wangapi, hawezi hata kueleza, nikamuuliza wajumbe wanaitwa  kina nani, hawajui.

“Nikamuuliza kama ana sheria za usalama barabarani, akasema hana na hata wajumbe wa baraza lake  hawana nakala za sheria.

“Hii inaonyesha   Serikali haina baraza la usalama barabarani la taifa ambalo linasimamia mabaraza ya mikoa na wilaya na linalofuatilia utendaji kazi wao.

“Kwa hiyo  nimeridhika kwamba  shughuli nyingi za usalama barabarani zilikuwa zinaendeshwa na watu wasiokuwa makini,” alisema Waziri Kangi.

Waziri Kangi pia alimuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi  (IGP), Simon Siro, kuhakikisha anafunga leseni za madereva wa mabasi na malori ambao wameonywa zaidi ya mara tatu kwa kukiuka sheria za usalama barabarani.

“Pamoja na hayo, wafutie madaraja ya C na E ukiwataka warudi darasani kusoma kwa sababu inaonekana hawajui wanalolifanya.

“Pia hakikisha Jeshi la Polisi linaendesha operesheni ya ukaguzi wa uhakiki wa leseni feki za madereva, kuwapima ulevi wakiwa hawajatoka kituo kikuu na kwenye vituo vyote vya mizani  huku ukaguzi wa magari hayo ukiendelea kufanyika.

“Nayasema haya kwa sababu tuna taarifa kwamba kuna askari wetu wasio waadilifu wanaohujumu vifaa vya kupima mwendokasi barabarani kwa kutopima baadhi ya magari na hata yakikamatwa, picha hizo hufutwa.

“Hivyo basi, askari atakayebainika akifanya vitendo hivyo afukuzwe kazi mara moja,”alisema.

Kuhusu mikoa yenye ajali nyingi za barabarani, alimtaka IGP Siro awachukulie hatua za  nidhamu maofisa na askari wazembe waliosababisha   ajali nyingi katika mikoa 10 ya  polisi.

“Katika kipindi cha mwaka 2017, Mikoa ya Ilala, Kinondoni, Temeke, Ruvuma, Shinyanga, Dodoma, Manyara, Tabora, Tarime/Rorya na Mbeya, imeongoza kwa ajali.

“Kwa hiyo  ni vema watendaji wake wakachukuliwa hatua za  nidhamu ili liwe fundisho kwa wengine wenye uzembe kama wao,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,474FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles