24 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wamachinga watengewe maeneo, wasibughudhiwe

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene

NA RAMADHANI HASSAN, DODOMA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene amezitaka halmashauri nchini kuwatengea maeneo wafanyabiashara wadogo   (machinga)   ili wasibugudhiwe kama alivyoagiza Rais John Magufuli.

Simbachawene alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema ).

Mbilinyi aliuliza ni kwa nini serikali haiweki mazingira mazuri kwa wamachinga.

Alisema  tatizo la wamachinga si kutengewa maeneo bali ni mazingira rafiki kwa wafanyabiashara hao.

Simbachawene alisema wamachinga hawapaswi kubughudhiwa bali kutengewa maeneo na suala hilo lilikwisha kuagizwa na Rais na halmashauri zote zina maelekezo.

Alikubaliana na mbunge huyo kuwa wamachinga hata wakijengewa majengo mazuri hawawezi kwenda kama si mazingira rafiki kwao kutokana na kuangalia wateja wao wanapatikana wapi.

Katika swali la msingi,  Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma (CUF),  alitaka kujua Serikali inatekelezaje agizo la Rais Magufuli na kwa kiasi gani.

“Rais akiwa Mwanza alipiga marufuku na kuziagiza mamlaka zinazohusika kuacha kuwasumbua wafanyabiashara  wadogo kama machinga,”alisema Nachuma.

Akijibu swali hilo la msingi, Naibu Waziri, Tamisemi, Selemani Jafo alisema mantiki ya agizo la Serikali la Rais akiwa Mwanza ilikuwa ni kutowahamisha wafanyabiashara wadogo katika maeneo waliopo endapo hakuna maeneo mbadala yaliyotengwa kwa ajili ya biashara zao.

Alisema mikoa na halmashauri imeendelea kutimiza malengo ya kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wadogo kwa kutenga maeneo rasmi ya kufanya biashara.

Naibu Waziri alisema maeneo yaliyotengwa rasmi kwa wamachinga katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara ni Likonde, Mbae, na Mjimwema.
Jafo alisema halmashauri inaboresha soko la Skoya ambalo halitumiki muda mrefu kutokana na kujaa maji ya mvua na kazi zitakazofanyika ni kurekebisha mitaro ya kupitisha maji  eneo hilo liweze kutumika kama ilivyokusudiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles