Na Aziza Masoud, Dar es Salaam
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema majina ya watu waliojiandikisha zaidi ya mara moja katika Daftari la Wapigakura, yamekabidhiwa kwa vyombo vya dola ili taratibu za kisheria zifuatwe ikiwamo kuwapeleka mahakamani.
Akizungumza katika kituo cha uchakatuaji (maandalizi) wa vitambulisho vya wapigakura jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima, alisema sheria inawataka watakaotiwa hatihani kutumikia kifungo au kulipa faini.
Aidha alisema kuwa endapo muhusika atahukumiwa kifungo kuanzia miezi sita atapoteza sifa ya kupiga kura katika uchaguzi ujao.
Mkurugenzi huyo alisema, idadi ya waliojiandikisha zaidi ya mara moja imefikia 52,780 kutoka 52,000 idadi ambayo ilitangazwa awali.
“Awali tulisema watu wanaojiandikisha zaidi ya mara moja hawataweza kupiga kura na tutawakamata tu kupitia mfumo wetu, waliofanya hivyo wajue wamefanya kosa la jinai.
“Hadi leo (jana) asubuhi tumewagundua watu 52,780 waliojiandikisha zaidi ya mara moja, wengine mara sita na wengine mara saba,” alisema Kailima.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo wa uchaguzi, idadi ya watu waliojiandikisha nchi nzima hadi sasa ni milioni 23.7.
Akizungumzia kuhusu malalamiko ya walemavu wa macho wanaodaiwa kutengwa katika zoezi la kupiga kura, alisema viongozi wa kundi hilo walifika ofisini hapo Jumanne ya wiki hii kwa lengo la kutafuta njia sahihi ya kuwasaidia waweze kupiga kura.
“Tumepanga kuwawekea utaratibu wao kuna kamati ambayo imeundwa na wenyewe watapanga njia nzuri ya kuwawezesha kupiga kura ikiwemo kutengeneza karatasi maalumu ambazo zitagharimiwa na tume,” alisema Kailima.
Akizungumzia kuhusu raia wa kigeni waliojiandikisha, Kailima aliwataka watu hao kuvisalimisha vitambulisho vyao katika ofisi za kata, wilaya na mikoa kabla ya kuchukuliwa kwa hatua za kisheria.
“Mashine ina utaratibu wa kutambua mtu aliyejiandikisha na sio raia kwa kushirikiana na watu wa uhamiaji kuna watu wamepingwa na mfumo si raia, nawapa siku saba wakabidhi vitambulisho katika ofisi za serikali,” alisema Kailima.
Alisema hakuna raia wa kigeni atakayefanikiwa kupiga kura na endapo NEC itaamua kumfuata mtu aliyejiandikisha na hakustahili atafikishwa katika vyombo vya sheria.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Daftari la Wapiga kura Dk. Sisti Karia aliwatoa hofu wananchi na kusema kuwa hakuna kura haramu zitakazoongezwa.