27.9 C
Dar es Salaam
Monday, February 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge amlilia Samia kuondoka kwa Lowassa

laizerPatricia Kimelemeta, Namanga

ALIYEKUWA Mbunge wa Longido, Michael Lekule Laizer, amemweleza mgombea mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, kwamba kitendo cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhama chama hicho, kimegawa wananchi wa jimbo hilo.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Namanga mkoani Arusha, Laizer alisema baada ya jina la Lowassa kuenguliwa kwenye wagombea wa CCM na kuamua kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baadhi ya wananchi wamemfuata kwenye chama hicho licha ya kujaribu kuwaelimisha sababu zilizofanya kada huyo aenguliwe.
Alisema mbali na kundi linalomuunga mkono Lowassa, wengine wamebaki CCM wakisema kiongozi huyo hajawahi kuwasaidia kitu.
“Wananchi wa Longido wamegawanyika kwa kitendo cha Lowassa kukatwa kwenye nafasi ya urais na kuhamia Chadema, jambo ambalo limewafanya wengine kumfuata,” alisema Laizer.
Alisema wananchi wa jimbo hilo hawana matatizo na CCM wala madiwani wa chama hicho, bali wana matatizo na mchakato mzima wa uteuzi wa majina ya wagombea ulivyofanyika kwa sababu hawajui utaratibu gani unaotumika uliosababisha kukatwa kwa jina la Lowassa.
Laizer aliwaambia wananchi hao kuwa, Kamati Kuu ya CCM ndiyo yenye jukumu la kupitisha jina la mgombea wa urais wa chama hicho.

Viongozi wa juu wa CCM, wakiwamo Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilali pia ni miongoni mwa waliondolewa.
Laizer alisema baada ya kuwaambia wananchi hao, baadhi yao walimwelewa, lakini wengine hawakumwelewa, hali iliyosababisha kujitokeza kwa mgawanyiko huo.
Alisema mtu anaamua kuondoka kwa uamuzi wake, lakini shughuli za chama zitabaki kama ilivyokuwa, hivyo basi aliwataka wananchi hao kuwa na umoja ili kuhakikisha CCM inapata ushindi, jambo ambalo linaweza kuwasaidia kupata maendeleo.
“Maendeleo hayawezi kuletwa na upinzani bali yanaletwa na wananchi kupitia CCM, hivyo basi tunapaswa kuungana na kuhakikisha mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia CCM anapata ushindi ili aweze kuleta maendeleo,” alisema.
Alisema katika kipindi hiki ambacho ameamua kupumzika, atashirikiana na mgombea huyo pamoja na wana CCM wenzake kuhakikisha ushindi unapatikana.
Kwa upande wake mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan, alimtaka Laizer kuwaelimisha wananchi wa jimbo hilo ili waweze kukichagua chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema mkakati wa Serikali ni kujenga hospitali ya wilaya katika jimbo hilo ili wananchi waweze kupata huduma ya afya.
Alimshukuru Laizer kutoa ofisi ya mbunge na kugeuza mahakama ya mwanzo na wilaya ili watendaji wa mahakama waweze kutimiza majukumu yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles