24.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Wanasheria wavalia njuga Masha kunyimwa dhamana

Laurence MashaNa Elias Msuya

CHAMA cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), kimelaani kitendo cha mwanachama wake ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, kunyimwa dhamana mahakamani.

Katika taarifa yake iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, TLS imesema mahakama imekuwa na tabia ya kunyima watu haki yao hiyo kwa kisingizio cha kuhakiki nyaraka za dhamana.

Kutokana na hali hiyo, chama hicho kimesema kitaunda tume maalumu ya kuchunguza uvunjwaji wa taratibu za mahakama unaosababisha watu kukosa haki za dhamana.

Masha ambaye pia ni wakili, alikamatwa hivi karibuni Kituo cha Polisi Oysterbay, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, alipokwenda kuwawekea dhamana vijana waliokamatwa kwa kosa la kukusanyika kinyume cha sheria.

Inadaiwa kuwa Masha alitoa lugha ya matusi kwa askari aliowakuta katika kituo hicho, hivyo naye akakamatwa na kuwekwa mahabusu kabla ya kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako alinyimwa dhamana na kupelekwa gereza la Segerea.

Rais wa TLS, Charles Rwechungura, alisema katika taarifa hiyo kuwa kumekuwa na tabia ya mashtaka huchukua muda mrefu kushughulikiwa na mshtakiwa anatakiwa abaki rumande akiwa na dhamana yake mfukoni.

“Tunalazimika kueleza hisia zetu kama wanachama wa kundi hili kutokana na tukio la hivi karibuni la kuomba dhamana kwa mmoja wa wanachama wetu. TLS inalaani bila kujuta na bila kuomba radhi kwa tabia hiyo ya aibu ambapo mwanachama wetu Lawrence Masha (Wakili) alifanyiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu,” alisema Rwechungura.

“Kosa alilokuwa akishtakiwa Masha la kutoa lugha chafu kinyume cha Kifungu cha 89(1) (a) cha Kanuni ya Adhabu [Cap 16 R.E.2002] linaangukia katika kundi la makosa madogo yanayotolewa dhamana,” aliongeza Rwechungura katika tamko hilo.

Alisema kutokana na ukiukwaji huo wa taratibu za mahakama, TLS itaunda tume maalumu ya kukusanya taarifa ili kukomesha tabia hiyo.

“Tanganyika Law Society itaunda tume maalumu ya kukusanya taarifa za kutosha iwezekanavyo kwa uvunjifu wa taratibu za mahakama katika utoaji wa dhamana, ili kuushirikisha mhimili wa mahakama kurejesha hali ya kawaida,” alisema Rwechungura.

Hata hivyo, alisema TLS haihoji kukamatwa kwa Masha na kama ni mkosaji au kosa aliloshitakiwa litachukuliwa kwa uzito gani na mahakama, bali wanacholalamikia ni kitendo chama mahakama kusababisha Masha kukosa haki yake ya dhamana.

“Wala TLS haihoji masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama kwa sababu kwa maoni yetu kwa masharti hayo yangesaidia. Tunacholalamikia na kukosoa ni uhalali na umakini wa mahakama kuacha jukumu lake na kusababisha Masha kukosa haki yake ya dhamana,” alisema.

Alisema wakati wote TLS imekuwa ikikemea kupitia matukio mbalimbali vitendo vya wazi vya kudharau mahakama na hasa pale mahakama inajikuta kwenye mazingira kama hayo.

“Kama wanachama tumeshuhudia mambo tunayoweza kusema yamekuwa yakirudiwa, yakihusisha mahakama na waendesha mashtaka ya kukataa kutoa dhamana kwa watuhumiwa wanaofikishwa mahakamani.

Kuna utaratibu mpya ambao haujaandikwa popote umeanzishwa ambapo mahakama inatoa haki kwa mkono mmoja na kwa mkono mwingine kumrudisha kwenye mashtaka kwa kisingizio cha kuhakikisha vielelezo,” alisema Rwechungura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles