24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mama Lowassa: Kwanini wamtungie mume wangu uongo? Waniulize mimi

0D6A4964NA AGATHA CHARLES, DAR ES SALAAM

MKE wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Regina, amesema anashindwa kuelewa ni kwanini watu wanatunga uongo kuhusu mumewe.

Akizungumza katika mkutano na wanawake kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Regina alisema yeye ni mtu pekee anayemfahamu mumewe kuliko  mwingine yeyote.

“Huyu ni mume wangu, namfahamu kulikoni mtu mwingine yeyote… ni mchapakazi, ni mtu anayethamini utu, mpenda maendeleo, asiyependa unyanyasaji. Nashindwa kuelewa kwanini watu wamtungie uongo badala ya kuja kwangu kuniuliza,” alisema.

Akizungumza huku akishangiliwa na wanawake waliohudhuria mkutano huo na kulazimu mshereheshaji muda wote kuingilia kati kuwaomba kunyamaza, Regina alisema kila mmoja afanye mabadiliko pamoja na kufika viwanja vya Jangwani kesho ambapo uzinduzi wa kampeni za Ukawa utafanyika.

Regina alisema kuwa amefarijika kuzungumza na wanawake na mabinti wa Tanzania kwa kuwa wao ndio chimbuko la maendeleo.

“Taifa linapaswa kufanya mabadiliko ya kweli ili kufikia maendeleo, na yatafanywa na wanawake… Kuna sheria nyingi ambazo zinamnyima mwanamke nguvu kama vile sheria ya kumiliki mali, wakati umefika wa kufanya mabadiliko. Ni wakati wa mabinti kuacha kudhalilishwa, wakati umefika kina mama kumiliki mali, huduma bora za jamii,  afya, elimu nk,” alisema.

Alisema wanawake ambao wanazalisha zaidi kuliko wanaume hawana manufaa na mazao wanayoyapata kutokana na kushindwa kuwezeshwa.

“Nadhani kuna umuhimu wa kubadilisha sera za kilimo, ufugaji na hilo litasaidia mabadiliko, sensa inaonyesha wanawake ni wengi na hivyo ni jeshi kubwa tukiamua kuleta mabadiliko tunaweza,” alisema.

 

Lowassa: Haya si mapenzi ni mahaba

Akihutubia umati huo wa wanawake, Lowassa alisema anadeka  kutokana na mafuriko ya wanawake ndani na nje ya ukumbi huo ambayo yalisababisha rafiki yake kutoka Zanzibar kumweleza kuwa si mapenzi bali ni mahaba.

“Nadeka, hizi ni baraka za mwenyezi Mungu na sio mkono wa mtu, rafiki yangu wa Zanzibar aliwahi kuniambia haya si mapenzi bali ni mahaba. Sasa nawapeni kazi, nimekuwa mbunge kwa miaka 30, wanawake ni waaminifu,  wakisema wanakupa kura wanakupa, naomba mnitafutie kura, nataka kura za kutosha kuwashangaza Watanzania, sio kura yako tu bali pia ya mume, watoto na mtu mwingine,” alisema.

Lowassa ambaye muda wote alikuwa akishangiliwa, alisema kuna ambao wanaona kuwa ameingia kwenye mchezo kwa kucheza, na kwamba watashangazwa na sanduku la kura Oktoba 25.

“Kila mwanamke anayenisikiliza naomba anipatie kura na tukimaliza kazi ya kura tutakutana Arusha Ngurdoto Desemba kama tulivyo. Halima na Mbowe tumezungumza jambo hilo, tukae mahali tujadili mabadiliko maana yake nini, nataka kupeleka maendeleo kwa kasi ya ajabu,” alisema Lowassa.

Alisema mabadiliko nchini hayaepukiki, kwani mwaka 1995 Nyerere aliuambia mkutano wa Chama Cha Mapinduzi kuwa Watanzania wanataka mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje.

“Nawaambia wana CCM waje huku kuna raha, wasiogope waje, nawaalika watoke huko na siku ya Jumamosi mtaona wengi tu watakuja, namshukuru Mwenyezi Mungu anayenijalia kupata deko kutokana na mapenzi haya, nawatuma kazi kwani nguvu ya umma haiwezi kushindwa, na hii maana yake Oktoba 25 mtanipeleka Ikulu,” alisema Lowassa.

 

Duni: Serikali yetu itamheshimu mwanamke

Naye mgombea mwenza wa Ukawa, Juma Duni Haji, alisema Serikali watakayoiunda itahusika na kushughulikia kwa kina masuala ya wanawake ambao wamekuwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ukosefu wa huduma bora za afya.

“Hivi sasa duniani jumla ya watu ambao hawapungui bilioni 6, hakuna aliyezaliwa na mwanaume, kama kuna kiumbe kinachopaswa kuheshimiwa ni mama. Sijawahi kusikia mama amepewa likizo kwa kuzaa watoto kumi, au kupewa mafao kwa kuwa amezaa, matokeo yake anaishia kudhalilishwa, hivyo mnapaswa kutupa Serikali tuweze kufanya kazi,” alisema Duni.

 

Mbowe aibua staili mpya

Akizungumza katika ukumbi huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alizindua namna mpya ya kushangilia kwa wanachama wake ikiwa ni alama ya mageuzi ambayo itatumika kama tuzo kwa Lowassa.

“Naomba tuanzishe ishara ya mabadilko ambayo inatumika duniani, na kupitia ishara hiyo tutampa Lowassa tuzo,” alisema Mbowe huku akionyesha alama hiyo ya kupinduapindua mikono.

Alisema Lowassa ambaye ni mpango wa Mungu amesababisha Watanzania kupata weledi wa kusimama pamoja bila kujali dini, kabila wala vyama.

Alisema kazi ya mageuzi ambayo imeanzwa tangu mwaka 1992 ni kama safari ya kwenda Kigoma ukitokea Dar es Salaam ambayo ikifika Pugu wapo watakaoshuka na kupanda, halikadhalika vituo vingine hadi inapofika.

“Mungu anatenda mambo kwa wakati, Lowassa sio mpango wa Mbowe wala Mbatia, ni mpango wa Mungu. Mungu amekubali Lowassa atoke aje kutuunganisha, aunganishe kina mama wote, Watanzania, vyama na kuwa kitu kimoja. Mambo yote ngoma Jumamosi.  Tulikuwa tunakwazwa kuhusu uwanja wa kuzindulia kampeni, lakini sasa kitendawli kimekwisha naomba mje kwa maelfu,” alisema.

Alisema katika mikutano ya Chadema kina mama watatengewa eneo lao ambalo mwanaume hataruhusiwa kufika na kutakuwa na ulinzi ili wasisukumwe, na kushiriki kwa raha, amani na ustaarabu.

 

HALIMA MDEE

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA), Halima Mdee, alisema wanawake wana hamu ya mabadiliko kitu ambacho kiliwafanya wafike hapo mapema zaidi.

Aliwataka wanawake hao kutodanganywa tena na sera alizosema zimekuwa zikitumika kila wakati wa uchaguzi kuwalaghai.

“Wanawake tumekuwa tukidanganywa sana, lakini tunaamini Jumamosi ilani ya chama itaonyesha kwa vitendo kuwa tunataka kuwafanyia nini wanawake,” alisema.

 

MBATIA

Kwa upande wa Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia, alisema wanawake ni wengi na wanaweza kufanya maamuzi muhimu.

“Mmedhalilika na kunyanyasika kupitia chama kingine na kufikia kuitwa malofa na wapumbavu,” alisema Mbatia.

 

TASLIMA

Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Twaha Taslima, alisema wanawake wanapaswa kusikika zaidi na kuwa na msimamo na kutoa sauti zao ambazo ni sauti za wengi.

“Sauti za wengi ni za Mungu, ikiwa kina mama mtasema safari hii ni Lowassa hakuna atakayepinga, tuchague viongozi wa Ukawa bara na Zanzibar,” alisema Taslima.

 

HALI TETE

Wanawake hao walianza kuwasili ukumbini saa 3 asubuhi na ilipofika saa 7 mchana ukumbi ulikuwa umejaa na kusababisha watu wengine kushindwa kuingia ndani.

Walinzi walilazimika kusimama kwenye lango la kuingia ukumbini hapo kudhibiti watu wasizidi kuingia.

Saa 8 mchana mke wa mgombea urais wa Ukawa, Regina Lowassa, aliwasili eneo hilo na kuibua shangwe kutoka kwa wanawake waliokuwa ndani na nje ya ukumbi huo.

Baada ya Regina kuwasili, wanawake waliokuwa nje walionekana kuwa na shauku kubwa ya kutaka kuambatana naye hadi ukumbini.

Purukushani hiyo iliwazidi nguvu walinzi waliokuwa mlangoni na kusababisha watu kuingia ndani kwa nguvu.

Kutoka na hali hiyo, baadhi ya viongozi wa Chadema walifika eneo hilo na kujaribu kutuliza wanawake hao na kuwawekea televisheni nne ili waweze kuona kinachoendelea ndani ya ukumbi.

Saa 9:50 alasiri Regina akiwa ameongozana na Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Halima Mdee pamoja na viongozi wengine wa baraza hilo walitoka nje ya ukumbi.

“First lady (mke wa rais) mtarajiwa atawasalimia halafu tutaenda ndani na mtashuhudia matukio yote kupitia televisheni,” alisema Mdee.

Saa 9:56 alasiri, Regina alipewa kipaza sauti na kuusalimia umati huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles