KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
MFANYABIASHARA Boniface Mwita (49), mkazi wa Tabata Kimanga na mkewe Rosemary Jenera (41), wanefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutoa maneno hatarishi kwamba hakuna corona, Serikali inadanganya.
Washtakiwa hao walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Vicky Mwaikambo na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi,
Mkunde Mshanga akisaidiana na Wankyo Simon. Akisoma mashtaka, Wankyo alidai kuwa washtakiwa wanashtakiwa kwa kosa la kutoa lugha hatarishi ama yenye kushawishi jamii.
Wanadaiwa Machi 20, 2020 ndani ya Dar es Salaam, wakiwa kwenye usafiri wa umma – daladala la kutoka Tabata kuelekea Muhimbili lenye namba ya usajili T 119 DKS aina ya Toyota Coaster, walitoa matamshi hatarishi.
Inadaiwa walisema: ‘Ugonjwa wa corona Serikali inadanganya, hakuna ugonjwa wowote na imefunga mashule kwa kuwa haina pesa na ada za kusomesha watoto bure’.
Washtakiwa walikana mashtaka na Wakili Wankyo alidai upelelezi umekamilika wanaomba tarehe ya kuwasomea maelezo ya awali. Hakimu Mwaikambo alisema
makosa wanayoshtakiwa nayo yana dhamana, hivyo alikubali washtakiwa wadhaminiwe kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wenye barua na vitambulisho na wasaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 5. Washtakiwa wote walikuwa na wadhamini, kesi itatajwa Mei 6.