27 C
Dar es Salaam
Friday, May 27, 2022

Watuhumiwa kukwepa kodi ya vileo hatma yao kwa DPP

 KULWA MZEE -DAR ES SALAAM 

MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP) anaendelea kuyafanyia kazi maombi ya msamaha yaliyowasilishwa na washtakiwa wanaotuhumiwa kukwepa kodi ya vileo, kuisababishia Serikali hasara zaidi ya Sh bilioni 31.48 na kutakatisha fedha hizo. 

Kesi hiyo ilikuja jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashidi Chaungu. 

Akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika, wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa. 

Pia alidai washtakiwa waliandika barua ya kuomba msamaha kwa DPP ili kumaliza kesi na kwamba suala lao bado linafanyiwa kazi. 

Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Mei 5 kwa kutajwa. 

Katika kesi hiyo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Jaruma General Supplies Ltd, Lucas Mallya na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka 23 ya uhujumu uchumi, ikiwamo kukwepa kodi ya vileo, kuisababishia Serikali hasara zaidi ya Sh bilioni 31.48 na kutakatisha fedha hizo. 

Awali washtakiwa hao walisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Issaya wakidaiwa kusababisha hasara Sh 31,489,529,153.07. 

Washtakiwa ni Mallya, Happy Mwamugunda, Prochesi Shayo, Geofrey Urio, Mhasibu Tunsubilege Mateni na Mkaguzi wa Hesabu, Nelson Kahangwa. 

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Januari 2015 na Januari 7, 2020 Dar es Salaam, kwa pamoja waliongoza genge la uhalifu kwa nia ya kupata faida. 

Shtaka la pili hadi la saba linamkabili Mallya ambaye anadaiwa Juni 3, 2019 Dar es Salaam alighushi kutengeneza stempu ya ushuru akionyesha imetengenezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati si kweli. 

Anadaiwa alitoa nyaraka hiyo ya kughushi TRA akionyesha ni halali wakati akijua si kweli na katika shtaka lingine inadaiwa Januari 7, mwaka huu, Chang’ombe A, Temeke, Dar ea Salaam alikutwa na rola 93 za stempu zenye thamani ya Sh 80,516,000 alizochapisha bila kibali cha kamishna wa mapato. 

Mshtakiwa Lucas anadaiwa kati ya Januari 2016 na Desemba 31, 2019 Dar es Salaam, kwa kutengeneza stempu hizo za kughushi, alisababisha hasara kwa Serikali Sh 15,241,075,169, akikwepa kodi kiasi hicho cha fedha na shtaka la saba anadaiwa kutakatisha kiasi hicho cha fedha huku akijua zinatokana na zao la kukweka kodi. 

Shtaka la nane linamkabili Happy Mwamugunda ambaye ni Mkurugenzi wa Happy Imports Associates, anayedaiwa Januari 2017 na Desemba 2019 bila kusajiliwa na kamishna wa kodi aliingiza katoni 413 za drostdy wine zenye thamani ya Sh 24,780,000 na shtaka la tisa anadaiwa kukwepa kodi Sh 9,584,401,393. 

Mshtakiwa huyo katika shtaka la 10 anadaiwa katika kipindi hicho alisababisha hasara ya Sh 9,584,401,393 na shtaka la 11 anadaiwa kutakatisha kiasi hicho cha fedha huku akijua fedha hizo zinatokana na zao la kumwepa kodi. 

Shtaka la 12 linamkabili Proches ambaye anadaiwa Desemba 19 mwaka 2019 alisambaza bidhaa zilizowekwa stempu za kughushi, katoni 749 za wine 75CL zenye thamani ya Sh 98,670,000, katoni 594 za drostdy hof 37.5CL zenye thamani ya Sh 12,002,000, katoni 14 za cousins 75CL14 zenye thamani ya Sh 16,240,000 na katoni za Amalula 58 zenye thamani ya Sh 12,120,000 ambazo zote thamani yake ni Sh 139,032,000. 

Washtakiwa hao wanadaiwa katika shtaka la 13 walikwepa kulipa kodi Sh 38,827,276, shtaka la 14 walikwepa kulipa kodi Sh 2,359,342,542.07 na shtaka la 15 na 16 wanadaiwa kusababisha hasara ya jumla ya fedha hizo na 17 kutakatisha. 

Shtaka la 18 linamkabili Urio ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya GMU Group, ambaye anadaiwa Desemba 2018 kwa nia ya kukwepa kodi, aliwasilisha taarifa za hesabu za uongo TRA na kusababisha kukwepa kodi ya Sh 4,265,882,773. 

Mshtakiwa huyo anadaiwa katika shtaka la 19 na 20 alisababisha hasara ya kiasi hicho cha fedha na kutakatisha fedha hizo huku akijua zinatokana na zao la kukwepa kodi. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,454FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles