26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

Walioacha ARV’s wasakwa majumbani Singida

  • 85 wapatikana, warudishwa kwenye dozi

SEIF TAKAZA- MKALAMA

ZAIDI ya waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi 85, kati ya 120 ambao walifuatiliwa majumbani mwao katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida,  wamerudi kutumia dawa za kufubaza virusi vya ugonjwa huo (ARVs).

Hayo yamebainika  wakati wa kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani kilichofanyika mwishoni mwa wiki mjini hapa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudhibiti Ukimwi Wilaya ya Mkalama, Dia Kambi, ambaye pia ni Makamu Mwenyikiti wa Halmashauri hiyo, alisema wagonjwa wote ambao wamerudishwa hospitali wameanza kutumia dawa na wanaendelea vizuri.

“Waheshimiwa madiwani, Oktoba hadi Desemba mwaka jana, wagonjwa 120 waliofuatiliwa, ni 85 tu waliorudi kliniki ya tiba na matunzo,’’ alisema Kambi.

Alisema changamoto kubwa inayokabili huduma hiyo, ni pamoja na waathirika kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu madhara ya kuacha kutumia dawa za kufubaza virusi.

“Oktoba hadi Desemba 2018, wagonjwa ngazi ya jamii kutoka vituo afya Mkalama na Iambi, wamejengewa uwezo wa kutekeleza majukumu yao kupitia mafunzo ya siku tatu yaliyotolewa na asasi isiyo ya kiserikali ya EGPAF.

 “Ilifanyika kampeni ya Furaha Yangu, Novemba 23, mwaka jana katika Kijiji cha Nkalankala, kutekeleza agizo la Waziri Mkuu alilolitoa jijini Dodoma mwaka jana, iliyokuwa na kaulimbiu ‘pima jitambue, ishi’.

 Katika uzinduzi wa kampeni hii, watu 216 walijitokeza kupima, kati yao wanawake ni 109 na wanaume 107 na kati ya hao hakuna aliyepatikana na VVU.

“Hata hivyo, upimaji wa hiari wa VVU katika zahanati, vituo vya afya na hospitali kwa kipindi cha Oktoba  hadi Desemba, mwaka jana, watu 7,605 walipewa ushauri nasaha na kupima virusi, kati yao wanawake ni 4,739 na wanaume 2,866. Lakini 77 walikutwa na maambukizi, kati yao wanaume ni 30 na wanawake 47, sawa na asilimia 1.03.

“Kiwango cha maambukizi kimeshuka kwa asilimia 0.47 ukilingnisha na asilimia 1.5,’’ alisema.

Alisema changamoto zinazokabili sekta hiyo, ni pamoja na kukosekana kituo cha tiba na matunzo Kata ya Kikhonda, lishe duni kwa baadhi ya watu wanaoishi na VVU pamoja na mitazamo hasi juu ya janga la Ukimwi miongoni mwa wanaoishi na virusi.

Kamati hiyo, ilishauri watu wanaoishi na VVU wapewe kipaumbele katika suala la mikopo ya vikundi ili kuboresha maisha yao.

Diwani wa Kata ya Mwanga, Mohamedi Juma (CCM),  alisema waathirika wengine hawaendi katika vituo vya kutolea huduma, hivyo kufanya takwimu  kutokuwa na usahihi na uhakika.

Akifunga mkutano huo, Mwenyekiti Kambi aliwaagiza watoa huduma wa sekta hiyo kuhakikisha wanatoa takwimu sahihi za waathirika.

HALI HALISI

Unywaji dawa za ARV ni mojawapo ya malengo yanayosisitizwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Ukimwi (UNAIDS).

Shirika hilo linapendekeza kufikia mwaka 2020 asilimia 90 ya watakaopimwa na kukutwa na VVU wapate dawa na asilimia 90 ya waliopo kwenye tiba wawe na kiwango kidogo cha virusi kwenye damu.

Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Ukimwi, imekuwa ikielimisha jamii kupima afya zao ili kama wameathirika waanze kutumia dawa hizo.

Hata hivyo, wako baadhi ya watu waliothibitika kuishi na virusi na kuanza dawa hizo, lakini wameamua kusitisha matumizi hayo.

Ripoti ya uhakiki wa muda wa kati wa Mkakati wa Tatu wa Kitaifa wa Kudhibiti Ukimwi wa 2013/14 hadi 2017/18 inaonesha bado kuna tatizo katika matumizi ya dawa hizo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu 24 kati ya 100 wamebainika kuacha kutumia ARV.

Kulingana na ripoti hiyo, watu wamekuwa wakiacha dawa kwa sababu ya umbali mrefu wa vituo vya matibabu, kuhamahama na kupuuzia baada ya kupata nafuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles