27.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 21, 2024

Contact us: [email protected]

Lwakatare azua taharuki kuonekana CUF

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SAALAM

MBUNGE wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare (Chadema), amezua taharuki baada ya kuonekana katika ofisi ya Chama cha Wananchi (CUF) akiwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya.

Lwakatare aliyepata kuwa mwanachama wa NCCR-Mageuzi na baadaye kuhamia CUF akiwa Naibu Katibu Mkuu kabla ya kujiunga na Chadema, alionekana katika ofisi hizo juzi na picha yake kusambaa mitandaoni.

Picha hiyo ya Lwakatare akiwa na viongozi hao wa CUF, ilizua taharuki huku mijadala katika mitandao ya kijamii ikiwa ni kiongozi huyo amejiunga na chama hicho.

Akizungumza jana na MTANZANIA, Lwakatare alisema ni kweli alipita maeneo ya ofisi za CUF, ambako alialikwa na aliyekuwa Mbunge wa Micheweni, Shoka Khamis Juma ambaye nyumba yake iko karibu na ofisi hizo.

“Wakati nikiwa CUF, Shoka alikuwa rafiki yangu na hata sasa ni rafiki yangu sana, sasa alinialika kwenye dua nyumbani kwake, akaniomba niende kuitembelea familia yake ambapo nyumba yake iko karibu kabisa na ofisi za CUF.

“Kama ulishatembelea CUF, pale kuna mazingira ya wafanyabiashara, kila kitu ni vurugu kwenye ile barabara, kwa hiyo sehemu pekee ya kupaki gari ni sambasamba na ofisi za CUF kwa mbele.

“Hivyo rafiki yangu Shoka, alinipokelea pale nje mbele ya ofisi ya CUF nikaenda kwake tukala biriani na pilau, tulipomaliza sasa wakati ananisindikiza kumbe CUF walikuwa na kongamano pale tangu asubuhi na nasikia walimpokea na Silvester Kasulumbayi (aliyekuwa Mbunge wa Maswa Mashariki – Chadema).

“Sasa kumbe wakati sisi tunatoka, na wao CUF walikuwa wamemaliza kongamano lao na watu walikuwa wanatoka kwa wingi kwenye geti lile la CUF, kwa hiyo baadhi yao waliponiona wakasema ‘ooh naibu katibu mkuu wetu wa zamani’.

“Hivyo watu wakapata shauku ya kuja kwa kweli wakaja kwa hamasa kubwa na ‘spirit’ kubwa ya kutaka kuniona, na miongoni mwa waliokuja ni aliyekuwa katibu wangu msaidizi ambaye sasa ni katibu msaidizi wa Profesa Lipumba.

“Akaja akanikumbatia pale nje ya geti, akaniomba kwamba Profesa Lipumba yuko ndani ofisini, hivyo niende nimsalimie na wanachama wote waliokuwa wamenizunguka wakasisitiza niende.

“Sasa mimi kwa kawaida yangu sina fitna, majungu wala visasi na sina tatizo lolote, ndiyo nikaridhia, tukaingia ndani ya geti wakawa wanaimba nyimbo za CUF, wao wakabaki chini, nikapanda juu ofisini kwa profesa na aliponiona akafurahi sana, akainuka, akanisalimia na bahati nzuri alikuwa anaendelea na kikao na wabunge na baadhi ya viongozi wengine wa CUF, wote wakapata hamasa ya kunisalimia, ‘karibu bwana ofisi yako ya zamani’.

“Na mimi nikawaambia mwenda kwao sio mtumwa, nikawaambia nashukuruni kwa upendo wenu na ilikuwa saa 12 jioni, nilitumia kama dakika 10 pale,” alisema Lwakatare.

Kutokana na hilo, alisema hana mpango wowote wa kujiunga na chama hicho na kwamba yeye ni mwanachama wa Chadema na mbunge.

“Mimi nina chama change, ni mbunge. Hivi kweli inalipa mimi muda kama huu niwe na ndoto au njozi ya namna hiyo, niweke tu wazi kwamba mimi ni muumini wa siasa za kistaarabu, sipendi siasa za kutekana, kutukanana, kuumizana, ndivyo nilivyo na ndivyo ninavyoasalimiana na watu wa CCM na ACT-Wazalendo,” alisema.

Alisema kuna wakati alizushiwa kuwa anajiunga na CCM, lakini jibu alilolitoa kwa watu waliomhoji ni kuwa siku zote matendo ndiyo yanazungumza kuliko maneno.

“Taarifa ile kuwa ningeunga mkono juhudi ikajifia, hata hii najua itajifia yenyewe, nataka tu kuwaambia mimi siasa zangu ni za ‘principle’, niko vizuri ndani ya chama changu ambacho ndicho kilichonipeleka bungeni,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF bara, Magdalena Sakaya aliliambia MTANZANIA kuwa Lwakatare aliwapitia tu kusalimia na wala hajajiunga na chama chao.

Alisema hata walipojaribu kumshawishi ili arudi ndani ya chama hicho, alisema aachwe kwa sasa ana chama chake ambacho ni Chadema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles