Na TIMOTHY ITEMBE, RORYA
MKUU wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Simion Chacha, amemwagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Charles Chacha, kuwachukulia hatua za kisheria ikiwamo kuwafukuza kazi walimu wanaodaiwa kuwapa ujauzito wanafunzi.
Agizo hilo alilitoa juzi katika kikao cha baraza la madiwani kuhusiana na msimamo wa Serikali kwa wanafunzi ambao wanapata ujauzito shuleni kwamba hawana nafasi ya kuendelea na masomo na kuwataka wananchi kuungana na Serikali kupiga vita vitendo hivyo ili visiendelee kutokea.
Mkuu huyo wa wilaya alisema amepata tetesi kuwa kuna walimu kutoka Shule ya Msingi Nyamugere na Kirogo wanadaiwa kuwapa mimba wanafunzi wao, lakini cha kusikitisha hatua za kiuchunguzi hazijachukuliwa ili kubaini ukweli.
“Mimi nitoe agizo kwako wewe mkurugenzi wa Halmashauri ya Rorya ili ukawachukulie hatua walimu hao ambao wanadaiwa kuwapachika mimba wanafunzi wao shuleni, hatutaki kulea watu kama hao na kuwafukuza kazi itakuwa fundisho kwa wengine,” alisema Chacha.
Naye Diwani Kata ya Bukwe, Charles Wembe (CCM), alisema halmashauri hiyo kupitia madiwani wake wanatakiwa kuwa chachu kwa kutoa elimu na kusimamia sheria.
“Watoto wetu wanaharibiwa na baadhi ya walimu ambao si waaminifu, sasa kwa hali hiyo tunatakiwa kusimamia haki pasipo kuwatetea wahalifu,” alisema Wembe.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rorya, Chacha, alisema baadhi ya wazazi na walezi wa watoto wanaficha ukweli pale inapotokea kitendo huku wahusika wakikubaliana mitaani, ambapo kesi inapofikishwa mahakamani hukosa ushahidi.