25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

JNIA YAJIZATITI KUDHIBITI UGONJWA WA EBOLA

 

Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM


KITENGO cha Afya katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), kimeweka udhibiti madhubuti wa  kujikinga na usambazaji wa magonjwa ambukizi ukiwemo ugonjwa wa Ebola.

Ugonjwa wa Ebola unaosambazwa kwa virusi vya Ebola, husababisha homa kali inayoweza kuambatana na kutokwa damu mdomoni, puani, masikioni, machoni na sehemu nyingine za wazi na unaenea kwa haraka. Hivi karibuni  umetangazwa kutokea nchini Kongo na kusababisha vifo.

Akizungumzia kuhusiana na mikakati hiyo ya kupambana na magonjwa ambukizi ukiwemo wa Ebola jana uwanjani hapo, Ofisa Afya Mfawidhi wa JNIA, Dk. George Ndaki, alisema  wanatoa mafunzo kwa watumishi na wahusika wote wanaotumia kiwanja hicho katika kujikinga na magonjwa hayo.

“Sisi tumejiandaa vizuri na tumeshafanya jitihada zote, tumeshatoa maelekezo, mafunzo na kamati mbalimbali za kiwanja zimejipanga kudhibiti magonjwa yote ya kuambukiza, ikiwemo sisi wenyewe kujikinga na kuwakinga na abiria wote wanaotoka katika nchi hatarishi,” alisema Dk. Ndaki.

Akizungumzia kuhusiana na utaratibu ambao kiwanja kimeweka ili kuhakikisha abiria wenye maambukizi wanapokelewa kwa tahadhari, ni kwamba wanapowasili na ndege zinazotoka nje ya nchi zinazopakia abiria wanaosafiri kutoka katika nchi zinazoshirikiana na Kongo, hutakiwa kusafisha mikono kwa dawa maalumu mara waingiapo katika eneo la kuwasili.

Alisema abiria hao wanapoingia katika lango la kuwasili la abiria kutoka nje ya nchi, kumekuwa na mashine maalumu inaangalia joto la mwili na likizidi nyuzi joto 38 wanamtaka kutoa maelezo zaidi ya afya yake.

“Abiria wote wanapowasili hupita katika eneo maalumu ambalo wote hutakiwa kuosha mikono, lakini pia kuna mashine ambazo zimewekwa ili kuweza kuwatambua abiria ambao wanawasili wakiwa na hali ya joto isiyokuwa ya kawaida, mfano kuwa na joto la juu sana kuanzia 38oC, ukiachana na hilo kuna fomu maalumu ambazo abiria wanapowasili hujaza.

“… na pia taarifa kutoka kwa rubani wa ndege kama kuna abiria ana maambukizi kwenye ndege. Baada ya kumtambua mgonjwa, basi atapitishwa katika njia ya tofauti na abiria wengine na kupakiwa katika gari la wagonjwa na kupelekwa Hospitali ya Temeke,” alisema Dk. Ndaki.

Naye Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha, alitoa ufafanuzi juu taarifa za uwepo wa ugonjwa wa Ebola, ameeleza kuwa tayari JNIA wanazo taarifa za mlipuko wa ugonjwa huo na taratibu zote zimeshachukuliwa kwa kuwakagua abiria wanaotoka nje ya nchi.

“Kwanza kabisa kwa abiria wote ambao wanatokea katika nchi ambazo zinasadikika kuwa na maambukizi, wanapowasili wanakuwa sanitized (wanaosha mikono na dawa maalumu) ili wasiweze kuleta maambukizi ndani, lakini pia tuna thermo scanners  (mashine ambazo zinaangalia hali ya joto la mtu) anapowasili ambapo tunapogundua mgonjwa ana matatizo, tunapeleka isolation (Chumba cha wagonjwa wa kipekee) na baada ya hapo anapelekwa katika vyumba vya wagonjwa waliotengwa katika Hospitali ya Temeke,” alisema Rwegasha.

Katika hatua nyingine, Dk. Ndaki alisema mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote ambaye amebainika kuwa na ugonjwa wa Ebola kupitia JNIA.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles