24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WAKINA SIMBU WANA UWEZO WA KUWAFUTA MACHOZI

Na ZAINAB IDDY, DAR ES SALAAM

MICHUANO ya dunia ya mchezo wa riadha inatarajiwa kuanza Agosti 4 hadi 13, mwaka huu mjini Londan katika Uwanja wa Olimpik, huku Tanzania ikitupa karata yake ya kwanza Agosti 5, ikiwa inawakilishwa na wanariadha nane.

Katika mashindano hayo mwaka huu Tanzania itawakilishwa na wanariadha wa mbio mbalimbali, ambao ni Faulina Abdi atakayeshiriki mbio za mita 10,000, mbio za marathon zitakazowashirikisha Watanzania Alphone Simbu, Ezekiel Ngima na Stephen Huche aliayechukua nafasi ya Said Makula, wakati kwa upande wa wanawake wapo Sara Ramadhan na Magdalena Shauri huku Gabriel Gerald na Emmanuel Giniki watakaokimbia mita 5,000.

Inakumbukwa kwa mara ya mwisho Tanzania kushiriki mashindano hayo na kupata medali ilikuwa ni mwaka 2005, Helsinik, Finland pale Christopher Isengwe aliporudi na medali ya fedha kwenye mbio za marathon baada ya kumaliza katika nafasi ya pili.

Tangu hapo Tanzania imeonekana kuwa wasindikizaji kutokana na mara kwa mara kurejea nyumbani mikono mitupu, huku wanariadha wetu wakishindwa kuingia hata kwenye 10 bora.

Kitendo cha kwenda wanariadha nane kwenye mashindano hayo makubwa ni ishara tosha kuwa safari hii Tanzania imeweza kufanya kazi, kwani ni zaidi ya miaka 10 sasa Tanzania imeshindwa kupeleka wanariadha wengi kwenye mashindano ya kimataifa.

Lakini pia hakuna asiyefahamu kuwa kabla ya Jumanne wanariadha hao kukwea ndege kwenda Londan, waliweza kuweka kambi mjini Arusha si chini ya mwezi mmoja na nusu kujiandaa na mashindano hayo ikiwa chini ya kocha Zakaria Berie.

Hivi karibuni tu kijana mdogo wa miaka chini ya 18, Francis Damin, aliweza kuing’arisha Tanzania katika mashindano ya Madola, haitapenda kaka na dada zake kutoka mikono mitupu London.

Litakuwa jambo la ajabu kuona kijana mdogo ameweza kuwatoa kimasomaso Watanzania halafu kaka na dada zake wenye uzoefu kimataifa kutoka patupu.

Hakuna asiyefahamu kiwango cha wanariadha wanaokwenda London kimataifa, hiyo imani iliyojengeka katika mioyo ya Watanzania inastahili kulindwa na vijana hao.

Haipendezi na haitaleta picha nzuri Tanzania iliyowahi kutoa wanariadha bora kimataifa na kuweka rekodi mbalimbali katika miaka ya1990 kama Seleman Nyambu, Filbert Bay na wengineo walipoweza kurudi na medali  huku rekodi zao hadi leo zikishindwa kuvunjwa.

Mbali na kuwa wanariadha mahiri, lakini pia watu hao wameshakuwa viongozi katika mchezo huo Tanzania wengine wakiwa na dhamana kubwa katika mchezo huo hadi sasa.

Simbu, Sara, Ngima, Magdalena na wengine, kama wanavyoaminiwa na Watanzania wanapaswa kuliangalia vizuri Taifa lao kwa kukimbia huku wakijua wapo watatu wanawategemea.

Ni ukweli uliowazi kwa hivi sasa kwenye sekta ya michezo ni riadha pekee ndiyo inayoweza kubeba na kuitangaza Tanzania kimataifa, kwa wachezaji wake kurudi na medali za dhahabu na kuweka historia mpya.

Huu ni muda wa kuwaamini Simbu na wenzake kwani wana uwezo wa kuwafuta machozi Watanzania katika sekta  ya michezo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles