25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

NI WAKATI WA SIMBA, YANGA KULETA MAGEUZI

LIGI Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2017/18 inatarajia kuanza Agosti 26, mwaka huu ikitanguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii baina ya watani wa jadi timu ya Yanga dhidi ya Simba utakaochezwa Agosti 23, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba na Yanga ni kati ya timu kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na Afrika kwa ujumla kutokana na mara nyingi  kuwa wawakilishi wa nchi katika mashindano mbalimbali yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).

Timu hizo kongwe mara nyingi zinapokutana huleta msisimko kwa mashabiki wa timu hizo na kwamba uwanja hufurika kushuhudia mchezo unaohusisha timu hizo kongwe nchini.

Licha ya kuwa ni timu kongwe na zinazowakilisha nchi mara kwa mara katika medani ya kimataifa, bado ipo haja ya timu hizo kubadilika na kuleta mageuzi ya soka la Tanzania kwa kuwa na vikosi imara ambavyo vinaweza kusaidia kufikia mafanikio makubwa ya kutwaa mataji katika mashindano yanayoandaliwa na CAF.

Kwa mwaka huu, Yanga itaiwakilisha nchi katika mashindano ya Klabu Bingwa barani Afrika wakati Simba itawakilisha katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, jambo ambalo limekuwa si geni kwa timu hizo kongwe kutoka Tanzania kushiriki mashindano kama hayo yanayoandaliwa na CAF.

Sisi MTANZANIA tunaona ipo haja ya Simba na Yanga kubadilika na kuendana na mfumo na mabadiliko ya kisasa ya mchezo wa soka yanayoendana na wakati kwa kuwekeza katika kujenga vikosi imara vitakavyokuwa tishio katika Afrika na kupigiwa mfano kama ilivyo kwa timu kama TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Si katika vikosi pekee, bali pia kujenga miundombinu kama viwanja ambavyo vitawasaidia katika kuwaingizia mapato badala ya sasa hivi kukinga mikono kusubiria mapato yatokanayo na viingilio katika viwanja vinavyomilikiwa na Serikali.

Timu hizi kuwa na viwanja vyake kutazisaidia kupata fedha zao wenyewe zitokanazo na viwanja vyao, lakini pia kuepuka gharama za kukodisha viwanja vya kufanyia mazoezi.

Sisi MTANZANIA tunaamini kuwa Simba na Yanga zina ushawishi mkubwa na mashabiki wengi katika soka la Tanzania, hivyo wanaweza kufanya mageuzi makubwa na kuwa mfano kwa timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Bado Simba na Yanga zina nafasi ya kufanya mageuzi katika soka la Tanzania na wasikubali kupitwa kama ilivyokuwa kwa Azam ambao wameonyesha mfano kwa kuwa na uwanja wao ambao umekidhi vigezo vya mashindano yanayosimamiwa na CAF.

Ni imani yetu kuwa Simba na Yanga wanaweza kufanya mambo makubwa zaidi ya Azam kwa kushirikisha makampuni mbalimbali ambayo yatawekeza na kuzifanya timu hizo kuwa bora zaidi barani Afrika tofauti na ilivyo sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles