24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wakili Mwale asomewa mashtaka 42 ya utakatishaji fedha haramu

NA JANETH MUSHI, ARUSHA
WAKILI maarufu jijini Arusha, Medium Mwale na wenzake watatu, wamesomewa mashtaka 42 yanayohusu utakatishaji wa fedha haramu, kughushi nyaraka na kukutwa na mali zilizopatikana kwa njia za uhalifu.
Watuhumiwa hao walisomewa mashtaka ya awali jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mustapha Siyani kabla ya kesi hiyo haijapelekwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha kwa kuanza kusikilizwa.
Akisoma maelezo hayo ya awali, Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyakyomya, alidai mahakamani hapo kwamba, watuhumiwa hao walitenda makosa hayo kati ya mwaka 2009 na 2011 kwa nyakati tofauti.
Alidai kati ya makosa hayo 42, mtuhumiwa wa kwanza Mwale anakabiliwa na makosa 27, ikiwa ni pamoja na kuficha uhalisia wa mali ambapo anadaiwa kutumia Sh milioni 70 kununua shamba lililopo katika Kijiji cha Ekenywa wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Katika kuficha uhalisia wa mali, mtuhumiwa huyo anadaiwa kutumia Sh milioni 250 kununua gari aina ya BMW lenye namba za usajili T 907 BTS na dola za Marekani 330,000 alizonunulia gari aina ya Landrover Discovery T 643 BTS.
Tibabyakyomya aliendelea kudai kwamba mtuhumiwa huyo pia alinunua nyumba mbili moja yenye thamani ya dola za Marekani 80,000, kiwanja namba 22 kilichopo Ilkiurei Arumeru na dola za Marekani 300,000 alizonunulia nyumba namba 21 eneo la Njiro jijini Arusha.
Wakili huyo wa Serikali aliendelea kudai kwamba Agosti 5, 2011, mtuhumiwa Mwale alikutwa na hundi tatu za Marekani zenye thamani ya dola 10,302, dola 10,333 na dola 95,079 ambapo kutokana na mazingira hayo zilionekana kuibwa ama zilipatikana kwa njia ya uhalifu.
Baada ya kutolewa maelezo hayo, Hakimu Mfawidhi Siyani aliwataka watuhumiwa hao kutojibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.
Katika kesi hiyo, upande wa Serikali uliiambia mahakama hiyo kwamba umejipanga kuwasilisha mashahidi 41 na vielelezo zaidi ya 42 kutokana na vingine kuendelea kuwasilishwa.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 2, mwaka huu ambapo upande wa Jamhuri watamalizia kuwasilisha vielelezo vya ushahidi wao mahakamani hapo.
Wakili Mwale alikamatwa mwaka 2011 na Jeshi la Polisi ambapo tangu wakati huo hadi sasa bado amekuwa akisota mahabusu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles