25.1 C
Dar es Salaam
Saturday, December 9, 2023

Contact us: [email protected]

Mwigulu: Nimetii amri ya Kinana

02NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba, amekiri kupokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, inayomtaka kutoendelea na ziara zake mikoani.
Kutokana na agizo hilo, amesema ametii agizo hilo la mkuu wake wa kazi na amelitekeleza kama alivyomtaka kufanya hivyo.
Akizungumza na MTANZANIA jana ili kupata ufafanuzi wake kuhusu barua hiyo ya Kinana iliyomtaka kukatisha ziara zake kama ameipokea na anaitambua, Mwigulu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, alisema agizo hilo ni halali kwa sababu ni la kiofisi, hivyo hana sababu ya kupingana nalo kwa mujibu wa utaratibu wa CCM na Serikali yake.
“Kwangu siwezi kupingana na agizo hilo halali la kiofisi, na pia ni agizo la bosi wangu ninayemsaidia kazi, na ninaamini kuna siku atanituma, na kuna siku ataniambia hiyo acha na mimi kazi yangu itakuwa utekelezaji maagizo,” alisema.
Alisema hatakuwa tayari kupinga maagizo hayo yaliyotolewa na Katibu Mkuu ambaye ni mkubwa wake wa kazi katika chama, na hivyo amesitisha ziara zake hadi pale atakaporuhusiwa.
Kauli ya Mwigulu imekuja siku moja baada ya kuripotiwa taarifa za kuandikiwa barua na Katibu Mkuu wa chama hicho, Kinana, aliyempiga marufuku kuendelea kufanya ziara ya kuzunguka katika wilaya na mikoa mbalimbali aliyokuwa akifanya kwa kutumia helikopta.
Katika barua hiyo ya Januari 18, mwaka huu ambayo ilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii, Kinana amemtaka Mwigulu kusitisha ziara zote na iwapo atataka kufanya ziara yoyote ya kichama, inambidi amuarifu na apate kibali chake.
Barua hiyo ilimlalamikia kwamba katika mikutano anayofanya amekuwa akionyesha mienendo na kauli zinazoashiria kujiandaa kugombea nafasi ya urais kupitia CCM.
Kinana alikwenda mbali na kueleza kwamba ziara za Mwigulu zimekuwa na mwelekeo wa kampeni jambo ambalo alidai ni kinyume na maadili ya chama chao.
Akizungumzia barua hiyo jana jijini Arusha, Kinana alikiri ofisi yake kumpa barua Mwigulu huku akigoma kueleza kwa undani suala hilo.
Juzi CCM kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa, Nape Nnauye, ilionya hatua ya baadhi ya makada wake kuanza kampeni.
Aidha chama hicho kimewataka wapambe na wagombea wao kuacha kutoa taarifa za uzushi dhidi ya makada sita wa chama hicho kwa lengo la kupotosha umma.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari visiwani Zanzibar, Nape alisema chama hicho kitawachukulia hatua kali makada wanaogombea na wapambe wao watakaobainika kusambaza taarifa za uzushi.
Pamoja na hali hiyo, CCM imewataka wagombea hao kuwadhibiti wapambe wao na kwamba wajichunge wenyewe dhidi ya hujuma kwa chama kwani zinaweza kuwapotezea sifa za kugombea.
Nape alisema pamoja na chama kutoa tahadhari kwa baadhi ya makada wake wanaotaka kugombea urais, lakini bado wameendelea na harakati hizo.
“Pamoja na kutotolewa kwa ratiba ya uchaguzi wa ndani ya chama, bado zimekuwapo harakati nyingi za wanaotaka kuteuliwa na CCM kugombea nafasi mbalimbali, hasa ya urais, ambapo baadhi ni halali na nyingine haramu,” alisema Nape.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles