ALLY BADI
WAKALA wa Ununuzi wa Serikali Mkoa wa Lindi, GPSA umekabidhi msaada wenye thamani ya Sh milioni moja kwa wagonjwa wa Hospitali ya Sokoine mkoani hapa.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Ununuzi Mkoa wa Lindi, Mwakiselu Mwambange, alisema wametoa msaada wa kanga, sabauni za kuogea na kufulia kwa wagonjwa pamoja na makopo ya maziwa kwa ajili ya kusaidia wagonjwa.
Mwambange alisema kitendo hicho ni utamaduni wa wakala wa ununuzi kusaidia watu wenye shida ikiwemo wagonjwa kwani wanaguswa na shida na matatizo waliyonayo wagonjwa hao.
“Kitendo hiki ni moja ya majukumu yetu kama wakala wa ununuzi kusaidia watu wenye matatizo kama hawa wagonjwa, tumeleta vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni moja kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa hao,” alisema Mwambange.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mganga Mfawidhi Dk. Evaristo Kassanga, alisema msaada huo utawezesha wagonjwa hao kuweza kujikimu na kuwasaidia kwa kipindi chote watakachokuwepo hospitalini hapo.
Dk. Kasanga, alisema kitendo kilichofanywa na wakala wa ununuzi kinahitaji kuigwa na wadau wengine kwani Serikali haiwezi kutoa huduma zote zinazohitaji kwa wagonjwa walioko hospitalini hapo.