Na Ramadhan Hassan, Dodoma
WAJUMBE 131 kati ya 177 wa Baraza la Chama cha Walimu Tanzania wamepiga kura ya kumsimamisha kazi Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Leah Ulaya kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kushindwa kusimamia, Taasisi, kanuni, katiba na maamuzi ya vikao.
Akizungumza Septemba 16,2021 na Waandishi wa Habari, Kaimu Rais wa CWT, Dinah Mathamani amesema katika kikao cha Baraza la Chama hicho kilichokaa juzi wajumbe wa baraza hilo walikubaliana kumsimamisha kazi,Ulaya kutokana na sababu mbalimbali.
Amesema uamuzi huo waliufanya kwa kupiga kura ambapo kura 131 zilikuwa ni za ndio,42 hapana na nne ziliharibika kati ya kura 177.
Amesema wajumbe hao walikubaliana asimamishwe kazi mpaka katika mkutano mkuu wa mwaka 2022 ndio utakaotoa maamuzi aendelee ama la.
“Baraza halina uwezo wa kumfukuza wenye maamuzi ya kumfukuza ni mkutano mkuu ndio maana wakakubaliana kumsimamisha,hajaachishwa bali amesimamishwa na baraza la jana halijafanya hivyo kwani kuna vikao,”amesema.
Amesema Ulaya alipewa nafasi ya kuzijibu hoja 13 ambazo ziliwasilishwa na walimu,Wesenslaus Leo ambaye aliwasilisha hoja tisa na Charles Chacha aliyewasilisha hoja 4.
Amesma majibu ya Ulaya hayawakuwaridhishwa wajumbe hao ambapo walikubaliana kumsimamisha kazi mpaka katika mkutano mkuu wa mwaka 2022.
Amezitaja hoja zilizoibuliwa na Leo na Chacha ni pamoja na kushindwa kusimamia kanuni,katiba na maamuzi ya vikao,kutoa lugha za kuchonganisha ngazi tofauti tofauti kwa kuitisha vikao ambavyo havikutambulika,kumwandikia barua Katibu Mkuu wa CWT kutaka watumishi wanne waliokuwa Makao Makuu wahamishiwe Wilayani.
Hoja zingine ni kugoma kufanya ziara pamoja na Kamati ya utendaji licha ya kupokea fedha kwa ajili ya ziara hiyo,pia karatasi zilizoonesha Ulaya awajibike hazikuonekana katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).